BANDA MEDIA BLOG

WANANCHI KIJIJI CHA LUGARI WILAYA YA MBINGA WAANZISHA MRADI WA UJENZI WA NYUMBA YA KUISHI WATUMISHI WA AFYA

 


Nyumba inayoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji cha Lugari wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuishi watumishi wa zahanati ya Lugari.

………….

Na Mwandishi Maalum, Mbinga

WANANCHI wa kijiji cha Lugari kata ya Mkumbi Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoa wa Ruvuma,wameanza ujenzi wa nyumba ya kuishi watumishi wanaofanya kazi katika zahanati ya kijiji  hicho kama sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lugari Devod Kapinga,amewashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kuanzisha ujenzi wa nyumba hiyo ambayo itawezesha watumishi  hao kuishi karibu na eneo la kazi hivyo kuwawezesha kutoa huduma za haraka kwa wagonjwa watakaofika kupata  matibabu katika zahanati hiyo.

Alisema,serikali imepeleka watumishi  kwenye zahanati hiyo,lakini changamoto kubwa iliyopo ni watumishi  hao wanaishi mbali na eneo la  kazi jambo linalosababisha baadhi ya wagonjwa kutopata huduma  kwa wakati.

“Baada ya wananchi kuona wanapata adha ya kutopata huduma za haraka,tulikaa kwenye vikao vyetu na tukakubaliana tuanze ujenzi wa nyumba angalau moja kwa ajili ya kuishi watumishi tulioletewa na serikali yetu,hata hivyo bado tumeshindwa kukamilisha kutokana na changamoto ya fedha kwani sehemu kubwa tunategemea fedha kutoka kwenye kilimo”alisema Kapinga.

Kwa upande wake Mganga kiongozi wa zahanati ya Lugari Dkt Theodora Robert alisema,kuanzishwa kwa mradi wa nyumba ya kuishi watumishi ni muhimu sana kwao kwani  wanapitia changamoto nyingi ikiwemo kuishi mbali na eneo la kazi na inapotokea mtu anapata dharura inakuwa vigumu kumuhudumia kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dkt Robert,katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi barabara nyingi zina utelezi  kwa hiyo inawawia vigumu kufika eneo la kazi kwa wakati unaotakiwa kitu ambacho wakati mwingine mgonjwa anapoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya haraka.

“Kwa hiyo kama nyumba hii itakamilika kwa wakati itusaidia sana sisi watumishi kufika eneo la kazi kwa wakati na wananchi kupata huduma ya haraka kwa sababu kwani tunapoishi mbali  ikitokea mgonjwa wa dharura inakuwa vigumu sana kuwahi hivyo kuona kama haujamtendea haki,kwa hiyo tukiwa karibu na eneo la kazi itamaliza kero  kwa wananchi wanaohitaji kuhudumiwa”alisema Dkt Robert.

Dkt Robert,ameiomba Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo  ili waweze kuishi karibu na eneo la kazi na kutoa huduma bora na za haraka kwa wananchi wanaokwenda kupata matibabu.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za wananchi Chama cha msingi cha ushirika Lugari Amcos kimechangia vifaa mbalimbali ikiwemo nondo na saruji vyenye  gharama ya Sh.milioni 1.5 ili kuendeleza ujenzi wa nyumba hiyo.

Katibu wa Chama  hicho Cornas Kapinga alisema,wameona ni vema kuunga mkono jitihada hizo zilizoanzishwa na wananchi kwani ndiyo wazalishaji wakubwa wa zao la kahawa linaloingiza mapato ya chama na kupitia ushuru  hivyo wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo.

Mkazi wa kijiji cha Lugari Damas Nchimbi alisema,walianzisha ujenzi wa nyumba ya wahudumu wa zahanati hiyo kwa nguvu zao,hata hivyo ameiomba Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na wadau wengine kuwaunga mkono ili nyumba hiyo ikamilike kwa wakati na wahudumu wapate sehemu salama ya kuishi.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG