BANDA MEDIA BLOG

WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA MAWASILIANO KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII

 

Wananchi wa kijiji cha Endadosh, kata ya Qash, wilayani Babati mkoani Manyara wamehimizwa kutumia huduma za mawasiliano kama nyenzo muhimu ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha na kusambaza miundombinu ya mawasiliano nchini.Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Devotha Minja (Mb), leo tarehe 23 Machi, 2026 wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyofanyika kwenye mnara uliojengwa katika kitongoji cha Maweni kilichopo katika kijiji cha Endadosh.

Mhe. Minja amesema, Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano ili kurahisisha shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kupata taarifa muhimu kuhusu masoko ya mazao yao, kubaini maeneo yenye mahitaji makubwa ya mazao, kufahamu bei katika masoko mbalimbali na kisha kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahali pa kuuza mazao yao ili kupata faida zaidi.

“Mawasiliano yana nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa wananchi. Ni muhimu kuyatumia kikamilifu ili kuboresha kipato na kuleta maendeleo katika familia na jamii,” amesema Mhe. Minja.

Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya mawasiliano kwa kuitunza na kuilinda dhidi ya vitendo vya uharibifu, akisisitiza kuwa miundombinu hiyo ni rasilimali muhimu inayowasaidia wananchi kupata taarifa, fursa za kiuchumi na huduma mbalimbali zinazochochea maendeleo.Kata ya Qash ni miongoni kata zilizonufaika na mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ya simu nchini. Katika kata hiyo, kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania imejenga mnara wa mawasiliano kwa ruzuku ya shilingi milioni 180 zilizotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF)

Kukamilika kwa mnara huo kunatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa Kata ya Qash na maeneo ya jirani, hali itakayochangia kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.     

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG