Na John Walter-Babati
Kongamano la wanawake kuelekea Siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa Machi 8, 2026, limefanyika katika Shule ya Msingi Vilima Vitatu, Kata ya Nkaiti, Wilayani Babati mkoani Manyara, likilenga kuhamasisha jamii juu ya haki na usawa kwa wanawake na wasichana.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati, limewakutanisha wanawake, wasichana pamoja na baadhi ya wanaume katika mdahalo wa wazi uliolenga kujadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa.
Maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050”, ikisisitiza umuhimu wa kujenga jamii inayotoa fursa sawa kwa wote kama msingi wa maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Januari Bikuba, amesema kuwa miaka ya nyuma wanawake walikuwa wakiachwa nyuma katika masuala mbalimbali ikiwemo umiliki wa ardhi, haki ya kurithi mali na kushiriki katika maamuzi ya kijamii na kiuchumi.
Amesema lengo la kongamano hilo ni kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa haki na usawa, sambamba na kuondoa mitazamo kandamizi inayowakwamisha wanawake na wasichana kufikia ndoto zao.
“Matamanio makubwa ya Dira ya Maendeleo ya Taifa hadi kufikia mwaka 2050 ni kuona wanawake wamejumuishwa kikamilifu katika nyanja zote za maendeleo, kisiasa, kiuchumi na kijamii,” amesema Bikuba.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Elimu kutoka shirika lisilo la kiserikali la So They Can (STC), Grace Swai, amesema kongamano hilo linaonesha namna ambavyo jamii imeanza kubadilika na kuelewa umuhimu wa kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu.
Amesema kwa sasa mwamko umeongezeka, wazazi wengi wanatambua thamani ya elimu kwa wasichana na wanachukua hatua kuhakikisha hawakosi fursa hiyo muhimu.
Washiriki wa kongamano hilo wameazimia kuendelea kuwa mabalozi wa haki na usawa katika maeneo yao, huku wakisisitiza kuwa ushirikiano wa wanawake na wanaume ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
