BANDA MEDIA BLOG

WAZIRI MKUU AAGIZA WATENDAJI WA ARDHI NCHINI KUTATUA MIGOGORO KWA UADILIFU NA WELEDI

 


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wote wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya ardhi kwa uadilifu na weledi ili kuondoa malalamiko ya wananchi yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne (Machi 10, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kasanga, Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Amesema kuwa katika maeneo mengi aliyopita, migogoro ya ardhi imeonekana kuwa miongoni mwa kero kubwa zinazowakabili wananchi huku ikichangia zaidi ya asilimia 90 ya malalamiko yanayowasilishwa katika mikutano ya hadhara.

“Nyinyi watu wa ardhi kama hamshtuki hata sasa, mnakaribia kuvunja udugu wetu. Hamshtuki? Sasa nataka haya mambo ya ardhi yamalizeni,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanazingatia maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu usimamizi wa ardhi.Amesema licha ya Serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji nchini, ni muhimu kuhakikisha haki za wananchi zinazingatiwa na kuepuka kuchukua ardhi yao bila kufuata taratibu.

“Mheshimiwa Rais amesema hata kama yeye ndiye anayeongoza na kuhamasisha uwekezaji, viongozi wote mikoani msichukue ardhi ya wananchi kiholela,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kina kuangalia namna migogoro ya ardhi inavyoshughulikiwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG