BANDA MEDIA BLOG

ZAIDI YA BILIONI 1 ZA MIKOPO YA ASILIMIA 10 ZA HALMASHAURI ZAWAINUA KIUCHUMI VIJANA KAGERA

 


Na Silivia Amandius 

Kagera.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, amesema zaidi ya shilingi bilioni 1 zimetolewa kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua iliyochochea kuinuka kwa vijana kiuchumi katika mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 28, 2026, Buruhani alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa operesheni maalum ya Vijana Daka Fursa na Samia, iliyofanyika katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuhamasisha vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Alieleza kuwa katika ziara hiyo, UVCCM ilitoa elimu kwa vijana kuhusu namna ya kuunda vikundi vya uzalishaji mali, kuandaa maandiko ya miradi yenye tija na kufuata taratibu sahihi za kuomba mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Buruhani, jumla ya vikundi 59 vya vijana vimefanikiwa kunufaika na mikopo hiyo, fedha ambazo zimewekezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, biashara ndogo ndogo na utoaji wa huduma.

 Amesema hatua hiyo imeongeza ajira na kipato kwa vijana wengi na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza elimu kwa vijana kuhusu fursa zilizopo ili kuhakikisha hakuna anayekosa mikopo hiyo kutokana na ukosefu wa taarifa au urasimu usio wa lazima.

Aidha, amewataka Maafisa Maendeleo katika halmashauri zote kutoka maofisini na kuwafikia vijana moja kwa moja, ili kuwasaidia kuandaa miradi bora na kusimamia ipasavyo mikopo wanayoipata.

Buruhani amehitimisha kwa kusema kuwa UVCCM itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati na kuwafikia vijana wengi zaidi, akisisitiza kuwa vijana wa Kagera wana uwezo wa kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG