BANDA MEDIA BLOG

DKT. NCHEMBA AZINDUA SERA YA UGAVI 2025, ASISITIZA UTAWALA BORA, UWAZI NA SHERIA

 NA MWANDISHI WETU,DODOMA

‎WAZIRI MKUU, Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa mamlaka, taasisi na wadau wote wanaosimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi na utawala wa sheria.

‎Akizungumza  Aprili 8, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre wakati wa uzinduzi wa sera hiyo kwa niaba ya Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema changamoto zinazoikumba sekta ya ununuzi wa umma hazitokani na sera au sheria zilizopo, bali ni uzembe na mitazamo ya baadhi ya watendaji.

‎Amesema taarifa za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zinaonesha wazi kuwa kasoro nyingi zinasababishwa na utekelezaji dhaifu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.‎“Sehemu kubwa ya changamoto hizi zinatokana na hulka, tabia na mitazamo ya watendaji. Hivyo, ni lazima tubadilike ili kufikia malengo ya sera hii,” alisisitiza.

‎Aidha, Waziri Mkuu ameitaka sekta binafsi kujipanga vyema kwa kuimarisha ushirikiano na sekta ya umma ili kunufaika na fursa zilizopo ndani ya sera hiyo mpya.

‎Amesema sera hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kipato kwa wananchi pamoja na kujenga uchumi jumuishi na shindani. 

‎Pia akiongeza kuwa Sera imeweka mwongozo mmoja unaounganisha hatua zote za mnyororo wa ugavi kuanzia ununuzi, uhifadhi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma.

‎Aidha, Waziri Mkuu, amebainisha kuwa sera hiyo pia inalenga kuimarisha matumizi ya rasilimali za ndani, kukuza viwanda vya ndani, kuendeleza teknolojia pamoja na kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

‎Katika hatua nyingine, amezitaka wizara, taasisi na mamlaka zote kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazokinzana na sera hiyo ili kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wake.‎Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema sera hiyo ni mwongozo muhimu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ugavi katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kudhibiti vitendo vya rushwa.

‎Amesema utekelezaji wa sera hiyo utaongeza ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

‎“Suala la mnyororo wa ugavi ni moyo wa uwajibikaji wa fedha za umma. Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa katika ununuzi na ugavi serikalini,” amesema Balozi Omar   

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG