Na:
Shambulizi hili lililolenga kituo hicho katika eneo la Asaluyeh, kinakuja baada ya rais wa Marekani kuonya kuwa Iran itashuhudia mashambilizi mazito katika miundo mbinu yake ya nishati, iwapo mlango wa Bahari wa Hormuz, hautafunguliwa kufikia siku ya Jumanne.
Katika hatua nyingine, Iran, imethibitisha kuuawa kwa Majid Khademi, mkuu wa kitengo cha ujasusi katika jeshi la ulinzi wa mapinduzi, baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa Marekani Jumatatu asubuhi.
Wakati hayo yakijiri, kombora la Iran limelenga makaazi ya watu katika mji wa Haifa nchini Israel na kuwauwa watu wanne, lakini pia ikishambulia miundo mbinu ya maji na nishati nchini Kuwait na Bahrain.
Mashambulizi mengine nchini Iran, yamesababisha vifo vya watu 34 wakiwemo watoto sita, huku Tehran ikisema imeandaa majibu yake kuhusu mapendekezo ya Marekani kuhusu kumaliza vita, huku ikisisitiza kuwa haitazungumza moja kwa moja na Marekani.
Ripoti za ndani zinasema, Mkuu wa Jeshi la Pakistan Asim Munir, amekuwa katika mawasiliano na Makamu wa rais wa Marekani JD Vance na mjumbe maalum wa rais Trump, Steve Witkoff na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbas Araqchi, kuhusu uwezekano wa kupata mkataba.