
Na Ssgt Mawazo Mtondo - Dodoma.
Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Aprili 20, 2026 amefungua rasmi mafunzo kwa Wakuu wa Magereza kuhusu Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu za Urekebishaji. Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu kuanzia leo Aprili 20 hadi 22, 2026 katika Ukumbi wa Rugimbana, uliopo Msalato jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo, CGP Katungu aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Alisema serikali imekuwa ikitoa rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya magereza, makazi ya watumishi, vyombo vya usafiri pamoja na kugharamia mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watumishi.
CGP. Katungu amebainisha kuwa moja ya majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ni urekebishaji wa wafungwa kwa kuwapatia Elimu, Ujuzi na Maarifa ili wanapomaliza vifungo vyao waweze kurejea kwenye jamii wakiwa na mchango chanya. Ameeleza kuwa jukumu la urekebishaji limebainishwa katika Kifungu cha 62 cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 pamoja na Kanuni Na. 404 ya Kanuni za Kudumu za Magereza za mwaka 2003 Toleo la 4.
Aidha, aliongeza kuwa mikataba ya kimataifa, ikiwemo Kanuni za Nelson Mandela na Tamko la Ouagadougou la mwaka 2002, pia zinasisitiza umuhimu wa urekebishaji wa wafungwa.
Katika kuimarisha utekelezaji wa jukumu hilo, Jeshi la Magereza limeendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuandaa mitaala mipya ya mafunzo kwa watumishi, kushirikiana na taasisi za serikali kama Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Chuo cha Uhasibu Arusha na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, pamoja na kuboresha miundombinu ya magereza.
CGP Katungu, alifafanua zaidi kuwa, mwongozo mpya wa urekebishaji umeainisha hatua nne muhimu katika mzingo wa urekebishaji (Rehabilitation Circle), ambazo ni mapokezi ya mfungwa gerezani, kipindi cha kutumikia kifungo na kupatiwa huduma za urekebishaji, maandalizi ya kabla ya kuachiwa huru na utengamanisho. Mwongozo huo pia unatoa fursa ya kufanya tathmini ya kina kwa kila mfungwa ili kumuweka katika programu stahiki kulingana na mahitaji yake.
Aidha, Jeshi linaangalia uwezekano wa kuweka utaratibu wa kuwawezesha wafungwa waliopata ujuzi wakiwa gerezani ili wanapotoka waweze kujiajiri na kujipatia kipato halali. Hatua hiyo inahusisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa serikali na inalenga kukamilisha mzingo wa urekebishaji na kuwawezesha wafungwa kurejea katika jamii kwa mafanikio.
“Ni matarajio ya uongozi wa Jeshi la Magereza kuwa mafunzo haya yatawawezesha washiriki kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mwongozo huu, jambo litakaloboresha huduma za urekebishaji kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisisitiza CGP Katungu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Usimamizi wa Wafungwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (ACP) Edith Mbogo, akitoa taarifa ya mafunzo hayo alieleza kuwa lengo la Mafunzo ni kuwawezesha washiriki kuelewa na kutumia ipasavyo mwongozo huo katika majukumu yao ya kila siku.
Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki watapata fursa ya kuongeza uelewa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha usimamizi wa programu za urekebishaji katika vituo vyao. Picha Ssgt Mfaume Ally




