Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Aprili 2, 2026
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani kimesema kinatambua mchango wa Serikali katika kuimarisha maendeleo ya mkoa huo, kufuatia ongezeko la bajeti kutoka Sh bilioni 473 mwaka wa fedha 2025/2026 hadi Sh bilioni 497.1 kwa mwaka 2026/2027.
CCM imeeleza kuwa ongezeko hilo ni neema kwa wananchi wa Pwani, kwani litasaidia kuboresha na kuongeza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 2, 2026, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoani humo, Dkt. David Mramba, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendeleza na kuuinua mkoa wa Pwani.
“Tunatambua mchango wa Rais wetu katika kuleta miradi ya kimkakati mkoani Pwani, hapo awali changamoto ya maji ilikuwa kubwa, tofauti na ilivyo sasa.”
” Ingawa bado kuna kukatikakatika kwa maji katika baadhi ya maeneo, hali hiyo inatokana na maboresho ya kiufundi yanayoendelea,” alisema Mramba.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi mingine unaendelea, jambo linaloonyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kuboresha maisha ya wananchi.
Katika sekta ya elimu, alieleza, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa madarasa ili kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi kujifunza.
Kwa upande wa afya, Dkt. Mramba alibainisha huduma zimeendelea kusogezwa karibu na wananchi kupitia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, hatua inayochangia kuimarisha afya ya jamii hususan mama na mtoto.
Kadhalika sekta ya usafirishaji imeimarika, ambapo barabara na reli zimeboreshwa, hali inayorahisisha usafirishaji wa mazao na huduma kwa wananchi
