Na Happy Lazaro, Arusha .
ZAIDI ya watengeneza maudhui 450 wakiwemo vijana wabunifu, wapiga picha, watayarishaji wa video pamoja na watumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii kutoka maeneo mbalimbali jijini Arusha wamekutana kwa lengo la kujengewa uwezo wa kibiashara na ujuzi wa kitaalamu unaolenga kuinua ubora ,ubunifu na uwajibikaji .
Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Kelvin Kanje, amewapongeza washiriki na kuwasisitiza kushirikiana na taasisi za Serikali na binafsi ili kukuza sekta hiyo inayokua kwa kasi nchini.
Aidha katika mafunzo hayo washiriki hao walipata fursa ya kupata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya usimamizi wa mikopo na uwekezaji kutoka Mfuko wa Utamaduni na Sanaa,msisitizo wa kulinda maadili na taarifa binafsi kwenye majukwaa ya kidijitali.
Aidha mafunzo mengine ni pamoja na wito wa kutumia sanaa kuhamasisha matumizi ya nishati safı ya kupikia kwa jamii.
Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha vijana na wabunifu wananufaika kiuchumi kupitia vipaji vyao.
Kanje amesema kuwa, awamu ya kwanza ya mafunzo kwa watengeneza maudhui mtandaoni imeanza rasmi mkoani Arusha, ikiwa ni hatua muhimu katika kuwajengea vijana ujuzi wa kitaalamu unaolenga kuinua ubora, ubunifu na uwajibikaji katika ulimwengu wa kidigitali unaokua kwa kasi.
Aidha washiriki hao wamepata nafasi ya kujifunza mbinu za kisasa za uandaaji wa maudhui yanayovutia hadhira, kuongeza ushawishi mtandaoni, pamoja na kutumia kwa ufanisi majukwaa ya kidigitali kufikia malengo binafsi na ya kibiashara.
“Mbali na kujikita katika ubunifu, mafunzo hayo pia yanasisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya kidigitali, ukweli wa taarifa na uwajibikaji katika utoaji wa maudhui, jambo linaloonekana kuwa msingi muhimu katika kujenga jamii yenye taarifa sahihi na salama mtandaoni.”amesema Kanje .
“Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuwawezesha watengeneza maudhui kutumia vipaji vyao kama fursa ya kujiajiri, kukuza kipato na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.”amesema Kanje.
Kwa ujumla, hatua hiyo inaakisi jitihada za kuimarisha sekta ya ubunifu nchini, huku ikiwapa vijana zana na maarifa yatakayowawezesha kushindana katika soko la kidigitali la ndani na kimataifa.
Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha vijana na wabunifu wananufaika kiuchumi kupitia vipaji vyao.



Tags
HABARI
