Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamefanya ziara katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kubadilishana na kujifunza namna ya uendeshaji wa miradi ya kimkakati kama vile hoteli pamoja na kumbi za mikutano zinazochangia kukuza uchumi na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri.
Katika ziara hiyo, Madiwani walipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo Ukumbi wa Mikutano wa Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba pamoja na Hoteli ya kisasa inayomilikiwa na Jiji la Dodoma, ambapo walijionea namna miradi hiyo inavyoendeshwa kwa tija na kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na serikali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Kuruthum Abdallah alisema kuwa wamevutiwa na kiwango cha uwekezaji pamoja na usimamizi madhubuti miradi hiyo na kubainisha kuwa Ilememla inakwenda kutumia uzoefu huo kama Darasa tosha.
“Tunaipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kumiliki na kuendesha miradi mikubwa na yenye tija kama hii. Sisi pia tuna miradi inayofanana na hii, hivyo ziara hii imetupa nafasi ya kujifunza mambo mengi ambayo tunaenda kuyafanyia kazi Ilemela ili tuweze kuboresha huduma na kuongeza mapato yetu ya ndani kupitia miradi ya kimkakati” alisema Abdallah.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Samson Medda alisema kuwa ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya halmashauri ni njia muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kuboresha utendaji wa taasisi za serikali za mitaa. "Tumekuja kujifunza na kuona kwa vitendo namna ambavyo Jiji la Dodoma limefanikiwa kuwekeza katika miradi yenye tija kwa wananchi. Maarifa na uzoefu tulioupata hapa utatusaidia kwenda kuongeza ubunifu, ufanisi na usimamizi bora wa miradi yetu ya maendeleo Ilemela” alisema Medda.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Neema Tambi alisema kuwa ziara hiyo imeongeza uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa miradi ya kimkakati katika kukuza uchumi wa halmashauri.
Ziara hiyo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inajenga taswira chanya ya ushirikiano baina ya mamlaka za serikali za mitaa.





