Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Kisare Makori katikati,akikabidhi mfano wa hundi ya Sh.milioni 111,332,600 kwa viongozi wa kikundi cha Vision Makers kilichopo kata ya Utiri Halmashauri ya mji Mbinga, wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa mwaka wa fedha 2025/2026,wa pili kushoto mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji Mbinga Amina Sefu,wa tatu kushoto Katibu Tawala wa wilaya hiyo Pendo Daniel na wa tatu kulia mwenyekiti wa CCM Wilayani humo Joseph Mdaka. 

Na Mwandishi Maalum,Mbinga

HALMASHAURI ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,imetoa mikopo ya asilimia kumi isiyo na riba ya Sh.milioni 325,468,700 kwa robo ya tatu na nne kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kutoka mapato ya ndani kwa vikundi 19 vya wanawake,vijana na walemavu vyenye wanufaika 201.

Akitoa taarifa wakati wa utoaji wa mikopo hiyo mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii mji wa Mbinga Cecilia Mbata alisema,kati ya fedha hizo Sh.186,332,600 fedha zilizokopeshwa kupitia asilimia kumi ya mapato ya ndani na Sh.139,131,100 zimetokana na marejesho kutoka kwenye vikundi 11 vya wanawake,vikundi 5 vya vijana na vkundi 3 vya watu wenye ulemavu.

Alisema,hadi kufikia mwezi juni 2026 jumla ya Sh.816,840,900 zimekopeshwa kwa kipindi cha dirisha la awamu ya kwanza na pili kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa vikundi 40.

Mbata alisema, katika fedha hizo vikundi vya wanawake 22 vimepata mkopo wa Sh.384,804,800,vikundi vya vijana 14 vimepata mkopo wa Sh. 413,336,100 na watu wenye ulemavu vikundi 4 ambavyo vimepata Sh.18,700,000.

Aidha alisema,hadi kufikia mwezi Juni 2026 vikundi vyote vilivyopata mkopo mwaka 2024/2025 na 2025/2026 jumla ya Sh.367,634,000 zilitakiwa kukusanywa kutoka kwenye vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

“Napenda kueleza kuwa,zoezi hilo limefanikiwa kwani hadi kufikia tarehe 30 Juni 2026 kiasi cha Sh.372,357,582 sawa na asilimia 101 zimekusanywa hivyo vikundi vyote vimerejesha vizuri na kwa wakati kwa mujibu wa sharia ya mikataba yao”alisema Mbata.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji Mbinga Amina Sefu,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuipatia Halmashauri hiyo fedha nyingi ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imewezesha wananchi kupata huduma bora za kijamii na kuweka mazingira wezeshi ya kiuchumi na kusimamia sera zinazolenga kuwainua wananchi wa kipato cha chini.

Amewapongeza wana vikundi waliopata mikopo hiyo kwenda kufanya kazi kwa bidii,kuwa na matumizi sahihi ya fedha walizopewa na wahakikishe wanarejesha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa watu wengine waweze kukopa.

“Nawaomba wale waliokosa kupata mikopo katika awamu hii wasikate tamaa bali wajitokeze kuomba kwenye awamu inayofuata kwani Halmashauri ya mji Mbinga inatoa mikopo kwa kila mwananchi anayehitaji”alisema Sefu.

Mkuu wa wilaya ya Mbinda Kisare Makori,amewataka wana vikundi hao kuwa na mipango mizuri ya biashara,kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati ili watu wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Amewasisitiza wanufaika,kuwa waaminifu,wabunifu na kufanya kazi kwa bidii kwani mikopo pekee haitoshi kuleta mafanikio bila kuwa na nidhamu ya fedha na usimamizi mzuri wa kazi wanazofanya.

Amewataka viongozi na watendaji wengine wa Serikali,kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia fedha zinazotolewa kwa makundi mbalimbali ziweze kutumika vizuri ili kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja,wilaya na Taifa.

Awali katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Pendo Daniel alisema,katika mchakato wa kupata walengwa wenye sifa walizunguka kwenye vikundi 19 vilivyopo katika kata 16 ili kujiridhisha kama vinastahili kupata mkopo wa asilimia kumi.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kurejesho upya mikopo hiyo baada ya kusitisha kwa muda ambapo amewasisitiza wanufaika kwenda kutumia fedha hizo kwa kazi iliyokusudiwa na kuepuka kutumia kwenye mambo ya anasa.