BANDA MEDIA BLOG

HUYU HAPA JAMAA ALIYEUBADILI UKRISTO MILELE!

                                                       ..................... 

​Mwaka 1517, mtawa mmoja na mwalimu wa chuo kikuu nchini Ujerumani alichukua msumari na nyundo, akapigilia karatasi mlangoni mwa kanisa. Bila kujua, kitendo hicho kidogo kilikuwa ni kiberiti kilicholipua mfumo mzima wa Ulaya, kuvunja ukuta wa miaka 1,000, na kuubadili Ukristo milele:

Jamaa huyu aliitwa Martin Luther.

​Hivi ndivyo alivyotikisa misingi ya dunia:

Katika karne ya 16, viongozi wa kanisa walikuwa wanauza karatasi maalum zilizoitwa Indulgences. Raia waliaminishwa kuwa ukinunua hati hizo, unanunua msamaha wa dhambi zako au za ndugu zako waliokufa ili watoke toharani kwenda mbinguni. Luther alikasirishwa sana na biashara hii akisisitiza kuwa msamaha wa Mungu ni zawadi ya bure kupitia imani, wala haununuliki kwa fedha!

Tarehe 31 Oktoba 1517, Luther alipigilia karatasi yenye Hoja 95 (95 Theses) kwenye mlango wa Kanisa la Wittenberg. Lengo lake lilikuwa kuanzisha mjadala wa kisomi tu, lakini wajanja walichukua maandiko hayo, wakayatafsiri, na kutumia mashine mpya ya kupiga chapa (printing press) kuyasambaza Ulaya nzima ndani ya wiki chache!

Papa na Mfalme wa Roma walighadhibishwa na Luther. Mwaka 1521, walimwita kwenye Baraza la Worms (Diet of Worms) na kumtaka afute kauli zake zote (recant) au auawe. Luther alitazama viongozi wakubwa na wenye nguvu zaidi duniani wakati huo na kusema kauli iliyoingia kwenye historia:

​"Dhamira yangu imefungwa na Neno la Mungu. Siwezi na sitafuta kitu chochote... Hapa ndipo niliposimama, siwezi kufanya vinginevyo. Mungu nisaidie."

Zamani, Biblia ilikuwa imeandikwa kwa Kilatini pekee—lugha iliyojulikana na viongozi wa dini pekee, hivyo wananchi waliamini kila walichoambiwa. Baada ya kukimbilia usalama wake kwenye Ngome ya Wartburg, Luther alijifungia na kutafsiri Biblia kwa Kijerumani cha mtaani. Kwa mara ya kwanza, raia wa kawaida waliweza kujisomea Neno la Mungu wenyewe! Kitendo hiki kilivunja mfumo wa zamani na kuzaa Uprotestanti (Protestantism).

​Mabadiliko makubwa hayaji kwa kufuata tu mikumbo na kukubali kila kinachofanyika. Wakati mwingine inahitaji mtu mmoja mwenye msimamo na ujasiri wa kusema "HAPANA" dhidi ya mfumo uliooza ili kuleta mapinduzi yanayowavua wengi kwenye kamba!

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG