BANDA MEDIA BLOG

ASKOFU WA KWANZA DAYOSISI YA KAHAMA KANISA ANGLIKANA AWEKWA WAKFU


Na Rev. Maiko Luoga – Kahama

Askofu Mkuu Maimbo Mndolwa wa Kanisa Anglikana Tanzania, Jumapili Tarehe 30 Agosti aliongoza Adhimisho la Misa Takatifu ya Kumweka Wakfu na Kumweka Kitini Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Kahama Capt. Esron Yuba Kaziri.

Akizungumza katika Misa hiyo Askofu Mkuu Maimbo, aliwataka waumini wa Dayosisi mpya ya Kahama kuwa wamoja ili kumsaidia Askofu Kaziri kutimiza kazi ya utume wa Injili pamoja na kuleta maendeleo ya Kanisa na Jamii.

Aidha aliwataka waumini hao kushiriki kazi za maendeleo ya Dayosisi ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Mtume Kahama, ambalo lipo katika hatua ya kupaua ili baada ya kukamilika lianze kutumika.

Akihubiri katika Misa hiyo, Katibu Mkuu wa Ushirika wa Kanisa Anglikana Ulimwenguni (Anglican Communion) Askofu Antony Poggo alisema, ni wajibu wa waumini kutoa muda na mali ili kumsaidia Askofu kutimiza malengo ya Dayosisi.

Alitoa wito kwa  viongozi wa Kanisa wakiwemo Maaskofu kutunza familia zao ili kuwa mfano wa kuigwa katika Kanisa na Jamii akisema, Askofu anapaswa kuwa Mume wa mke mmoja anaempenda mkewe na watoto ili kulinda Kanisa la Mungu.

Akizungumza na Washiriki wa Ibada hiyo, Askofu Capt. Esron Kaziri aliahidi kufanya kazi kwa umoja kati yake, wahudumu na waumini wa Dayosisi ikiwemo kueneza Injili katika maeneo tofauti kwa kupanda Makanisa Mjini na Vijijini.

Mgeni Rasmi katika Misa hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita aliye mwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kupitia Hotuba yake Mhe. Mboni alipongeza Kanisa Anglikana Tanzania kwa kuendeleza kuhubiri umoja, upendo na mshikamano nchini. 

Mhe. Mboni Mhita kupitia Ofisi yake aliahidi kutoa Fedha kiasi cha Shilingi milioni ishirini Ili kuwezesha kazi ya kupaua Jengo la Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Kahama na Dayosisi ya Central Tanganyika Kanisa Anglikana Tanzania kupitia Askofu Dickson Chilongani ameahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni Tano.

Dayosisi ya Kahama imezaliwa kutoka Dayosisi ya Tabora inayoongozwa na Askofu Elias Chakupewa ambae ametangaza rasmi kuachia eneo hilo ili lianze kujitegemea.














Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG