Na Rev. Maiko Luoga – Shinyanga
Askofu Johnson Chinyong’ole wa Dayosisi ya Shinyanga, Kanisa Anglikana Tanzania Jumapili Tarehe 6 Septemba 2026 aliongoza Adhimisho la Misa Takatifu ya kuamuru wahudumu Mashemasi 7 Makasisi 9 na kuwaingiza kazini Viongozi watatu wa Walei.
Akihubiri katika Misa hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Stephano Shinyanga, Askofu Chinyong’ole aliwaasa Wahudumu walioamuriwa, kutumika katika Kanisa la Mungu kwa wito wa kweli ili kutimiza wajibu wao.
“Mmeitwa, mnapaswa kuitika na kutumika kwa uaminifu shambani mwa Bwana, Nyakati hizi zimeambatana na mambo mengi, mnapaswa kutumika kufundisha na kukemea mambo mabaya” Alisema Askofu Chinyong’ole.
Misa hiyo ya Siku ya Bwana ya 15 baada ya Pentekoste na Utatu 14 yenye wazo Kuu Tunda la Roho, ilifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Stephano Shinyanga na kuhudhuriwa na wahudumu, waumini pamoja na wakristo kutoka ndani na nje ya Dayosisi ya Shinyanga.










