Na Joseph Ishengoma, MAELEZO
Askofu Mkuu wa jimbo kuu la
Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka kesho (tarehe 27.11.2015) anatarajia
kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye ziara ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa
Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis nchini Uganda.
Baba Mtakatifu Francis
anatarajia kuwasili nchini Uganda kesho kwa ziara ya siku mbili akitokea
Kenya kabla ya kuelekea Afrika ya Kati.
Hii ni ziara ya kwanza kwa
kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kutembelea Bara la Afrika
tangu alipoliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013.
Katibu wa Baraza la Maaskofu
(TEC) nchini Padre Raymond Saba amesema Mabaraza ya Maaskofu ya Kenya
na Uganda kwa pamoja yalitoa mwaliko kwa TEC kushiriki katika ziara ya
Baba Mtakatifu katika nchi hizo.
“Tulipata mwaliko kutoka Kenya
na Uganda, lakini tumeangalia nafasi yetu na jinsi ya kushiriki katika
ziara hii. Hatukuweza kutuma mwakilishi Kenya, lakini Askofu Ruzoka
ataiwakilisha TEC Uganda,” amesema.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, jana
mabasi mawili ya waumini wa dini ya Kikristo yaliondoka mjini Mwanza
kuelekea Namugongo, Uganda ambapo Baba Mtakatifu atakapofanyia ibada.
Eneo la Namugongo ndipo Mfalme Kabaka Mwanga II alipowachoma na kuwaua mashahidi 22 wa Uganda waliofia dini katika karne ya 18.
“Natoa wito kwa waumini wa
Kanisa Katoliki nchini, wafuatilie na kusikiliza kwa makini ujumbe wa
Baba Mtakatifu aliouleta katika Barani Afrika kwa sababu unagusa moja
kwa moja amani na ushirikiano miongoni mwa jamii,” amesema.
Kwa mujibu wa Padre Saba, Baba
Mtakatifu hufanya ziara kufuatia mwaliko wa kanisa na serikali ya mahali
husika au tukio la kimataifa linalohusiana na imani Katoliki.
Amesema, “Kanisa pekee yake
haliwezi kufanikisha ziara ya Baba Mtakatifu. Ndio maana alipofika Kenya
alipokelewa na Rais Uhuru Kenyatta na hata alipokuwa Marekani
alipokelewa na Rais Baraka Obama ingawa sio rahisi kwa kiongozi wa
Marekani kumpokea mgeni uwanja wa ndege.”
Ziara ya Baba mtakatifu nchini
Marekani ilipangwa kabla hajawa kiongozi Mkuu wa kanisa Katoliki. Ziara
hiyo ilitokana na kongamano la kimataifa la familia lililofanyika mjini
Filadelphia.
Papa Francis anatarajia kuhudhulia kongamano la vijana ulimwenguni nchini Poland mwaka 2016.
Tags
HABARI KITAIFA
