Ndugu zangu,
Imekuwa ni utamaduni wangu kutuma
salamu za Mwaka Mpya kwa wajumbe wangu wa Mjengwablog, marafiki zangu
kwenye FB na wengine walio ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Nimefanya hivyo tangu mwaka 2006 ilipoanzishwa Mjengwablog. Na mwaka huu naendeleza utamaduni huo.
Naandika salamu hizi nikiwa hapa Iringa, na nikiwa na mambo mawili ya kuwaeleza;
Mosi, napenda kuwahakikishia kuwa Mjengwablog/KwanzaJamii itaingia mwaka mpya wa 2016 na kasi zaidi ya mwaka jana. Tutazidisha ubunifu katika kuwaletea huduma mpya na bora zaidi.
Mosi, napenda kuwahakikishia kuwa Mjengwablog/KwanzaJamii itaingia mwaka mpya wa 2016 na kasi zaidi ya mwaka jana. Tutazidisha ubunifu katika kuwaletea huduma mpya na bora zaidi.
Ikumbukwe, Mjengwablog ilikuwa
blogu ya kwanza hapa Tanzania kuja na ubunifu wa kuweka kurasa za mbele
za magazeti mwaka 2007. Mwaka huu tumekuwa blogu ya kwanza Tanzania kwa
kuwa wa kwanza kila alfajiri kuwaletea habari za magazetini zikiwa na
uchambuzi wa habari ku 3 ikiwamo uchambuzi wa katuni bora ya siku.
Mwakani tumedhamiria kuunganisha
huduma hizo na radio blogging ikiwa na maana ya kufanya chambuzi kwa
njia ya radio ya mtandaoni na kuposti ( KwanzaJamii Radio). Mengine
mapya ya kiubunifu yako jikoni, yatakuja kwa mwaka ujao, 2016.
Jambo la pili nililotaka kulisema
linahusu hali ya mtanziko wa kisiasa Zanzibar. Ni majuzi tu nilikuwa
Zanzibar kwa takribani juma moja. Nilitembea Zanzibar mjini na vijijini.
Hakika, sijawahi kupanda boti na
kuviacha visiwa vya Zanzibar nikiwa na shaka ya kitakachotokea nyuma
baadae. Safari hii niliondoka Zanzibar nikijisikia hivyo. Zanzibar
sikuikuta hali njema ya upepo wa kisiasa. Nakumbuka nikiwa kitongoji
kimoja pale Jambiani nilioongea na wenyeji walioonyesha shaka kwenye
mazungumzo. yao wakati wakiongea nami.
Pale Jambiani niliiona chuki
baina ya wenyeji iliyotokana na tofauti za kiitikadi. Chuki
iliyoonyeshwa hata kwenye maandishi ya kutani na kwenye milango ya
nyumba. Ni chuki iliyoonyeshwa hata kwenye mijadala ya mitandaoni ambayo
binafsi niliianzisha kwa madhumuni ya kuamsha fikra na kubadilishana
maarifa na uzoefu.
Niliyoiona si Zanzibar
niliyoifahamu. Bado naamini, Zanzibar imejaa watu wakarimu na wenye
upendo. Suluhu ya Zanzibar itapatikana na Wazanzibar wenyewe na kwa njia
ya mazungumzo hadi kufikia muafaka.
Na walio kwenye meza ya
mazungumzo wasitangulize maslahi binafsi. Kwenye kujadiliana ili kutatua
mgogoro pande husika ziwe tayari kupata na kupoteza. Si vema pia kwenda
kwenye meza ya mazungumzo ukihitaji jambo moja tu, kwamba kama
ukilikosa ndio mwisho wa dunia.
Na duniani hapa mengine
yaliyofutwa, na kama ni kisheria na yakachapwa hata kwenye gazeti la
serikali, basi, si rahisi yakarejeshwa kwa wino ule ule. Ni vema
ikatangulizwa hekima na busara. Ni vema na ni busara yakawekwa mazingira
ya, hatma ya yote, kuwa pande zinazokinzana zote zikaibuka washindi.
Na hakuna namna yeyote ile ya
kuvifanya visiwa vikawa tulivu bila ya uwepo wa makubaliano ya Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ambapo viongozi wakuu wa pande zote mbili wafanye
kazi ya ziada ya kuwahimiza wananchi wao kuchimba makuburi marefu ya
kuzizika chuki zao baina ya wao kwa wao. Chuki zilizojengeka kwenye
misingi ya ubaguzi. Na sote tunajua dhambi ya ubaguzi, ni kama dhambi ya
mwanadamu kuonja nyama ya mwanadamu mwenzake, hawezi kuacha.
Ni iwekwe wazi, kuwa suala la
Muungano wetu halipaswi kuwa mjadala tena kama uwepo au usiwepo, bali ni
kwa namna gani tutauimarisha.
Maana, daima utabaki kuwa ukweli, kuwa jambo la Zanzibar ni letu Bara, na kinyume chake.
Maana, daima utabaki kuwa ukweli, kuwa jambo la Zanzibar ni letu Bara, na kinyume chake.
Na tuwe tayari kupambana hadi
risasi ya mwisho, na nguvu zote hasi, za ndani na nje ya mipaka yetu,
zinazotaka kututenganisha kwa misingi ya Uzanzibar, Upemba, Ubara na
hata udini.
Ni imani yangu, kama ilivyotokea huko nyuma, kuwa Zanzibar imeweza kuvuka mitihani migumu na ikasimama tena.
Naziona ishara za tumaini jipya
la Zanzibar linalokuja. Kwamba viongozi wakuu wa CCM na CUF Zanzibar
watazishinda nguvu hasi na zinazochagizwa na wahafidhina wa pande zote
mbili, hivyo, kupata formula mpya ya kuvivusha visiwa vya Zanzibar na
Pemba kutoka kwenye mtanzuko wa kisiasa uliopo sasa.
Mungu Ibariki Tanzania na Heri Ya Mwaka Mpya.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Tags
HABARI KITAIFA