Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard
Kasesela akipanda miti jana wilayani humo ikiwa ni sehemu ya uzinduzi
wa kampeni ya kupanda miti. Benki ya Diamond Trust Tanzania imedhamini
shughuli hiyo kwa kuchangia sh. milioni tano. Picha kwa hisani ya DTB.
……………………………………………………………………………………………………..
Na ImmaMatukio
BENKI ya Diamond Trust Tanzania,
imedhamini shughuli ya upandaji miti katika Wilaya ya Iringa iliyopo
mkoani Iringa kwa kuchangia sh. milioni tano. Wilaya ya Iringa imeanza
rasmi kupanda miti katika maeneo yaliyotengwa na uongozi wa wilaya,
ikiwa ni utekelezaji wa programu ya kitaifa ya kupanda na kutunza
mazingira inayoanza mwezi huu.
Wilaya ya Iringa inategemea kupanda zaidi ya miti 5,000 ya
mbao, mapambo, kivuli na matunda. Programu ya kupanda miti na kutunza
mazingira ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Maliasili na Utalii,Prof.
Jumanne Maghembe, wiki iliyopita.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard
Kasesela wakati akizindua kampeni ya kupanda miti jana alieleza kuwa,
Wilaya ya Iringa imetenga maeneo makubwa ya hifadhi ya misitu na
mazingira ili kuhifadhi na kuongeza kiwango cha maji nchini katika
tarafa za Mlolo, Ismani, Kalenga, Pawaga na Idodo.
Pia alisisitiza umuhimu wa miti
na misitu katika kuhifadhi maji na umuhimu wa maji kwa viumbe hai.
Alisema, upandaji miti na utunzaji wake utasaidia kupata hewa nzuri,
maji, mvua, kupunguza joto na kupambana na mabiliko ya tabianchi.
Programu hiyo ya kitaifa ni ya
aina yake nchini na inashirikisha serikali kuu, wananchi na sekta
binafsi. Akizungumza na waandishi wa habari walioshiriki katika shughuli
ya kupanda miti, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Diamond Trust
Tanzania, Ndugu Viju Cherian, alisisitiza umuhimu wa programu ya kupanda
miti.
Kutunza mazingira ni moja ya
nguzo kuu ya benki yetu katika maeneo tunakofanya biashara. Kwa
kuzingatia hilo, tumeitikia wito wa Mkuu wa Wilaya na kuunga mkono
programu hii kwa kuchangia shilingi milioni tano. Benki ya DTB ni
mshirika mkubwa katika hifadhi ya mazingira nchini kote,ö alisema.
Benki ya DTB ilifungua tawi
katika mji wa Iringa mwaka 2014 na hadi sasa ina matawi 24, matawi 10
yakiwa katika jiji la Dar es Salaam (tawi kuu la Dar es Salaam Mtaa wa
Jamaat, Masaki, Morocco,Magomeni, Mbezi, Mbagala,Barabara ya Nyerere,
Kariakoo, Barabara ya Nelson Mandela karibu na njia kuu ya Tabata na
Upanga katika Barabara ya Umoja wa Mataifa.
Pia ina matawi katika miji ya
Arusha, Mwanza, Zanzibar, Dodoma, Tanga, Mbeya, Moshi, Iringa, Morogoro,
Tabora, Kahama na Mtwara. Aidha, DTB ni mshirika wa Mfuko wa Maendeleo
ya Kiuchumi wa Aga Khan, ambao ni sehemu ya mtandao wa maendeleo wa Aga
Khan (Aga Khan Development Network).
Tags
HABARI KITAIFA
