Hayati Padri Calisti Nauli Nyambo
ELIMU YA MSINGI
Mwaka 1948 hadi 1953 alisoma
katika Shule ya Msingi Iwa hadi darasa la sita. Kwakuwa wakati ule shule
ya msingi Iwa ilikua na darasa la kwanza hadi la sita tu, Calisti
aliendelea na masomo ya darasa la saba kule milimani Usambara mwaka 1954
katika shule ya Msingi Gare. Mwaka 1955 aliendelea na masome ya darasa
la nane katika Shule ya Msingi Kichwele (au Uhuru) katika Jimbo Kuu la
Dar-es-Salaam.
ELIMU YA SEKONDARI
Mwaka 1956-1957 Calisti
aliendelea na masomo kidato cha kwanza na cha pili katika Shule ya
Sekondari Umbwe.Alifuzu vizuri masomo yake akachaguliwa kujiunga
na kidato cha tatu na cha nne katika Shule ya Sekondari ya Pugu Dar es
Salaam 1958 hadi 1959.
WITO WA UPADRE
Calisti aliongozwa na Roho
Mtakatifu alijisikia kuitwa na kuvutwa na wito wa Upadre.
Akaomba kujiunga na masomo ya Seminari kupitia Jimbo Katoliki Moshi.
Mwaka 1960 hadi 1962 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho.
Baada ya kuhitimu masomo ya
Falsafa, aliamua kukatiza masomo na malezi ya Seminari. Akaajiriwa
kufanya kazi Benki na Serikalini. Kutokana na nguvu ya wito wa Upadre
fedha za mshahara hazikutosheleza dhamira na malengo ya maisha yake ya
kupenda kumtumikia Mungu. Hivyo aliamua arudi Seminari kuendelea na
safari yawito wa Upadre.
Akaomba kujiunga na Jimbo Kuu la
Dar-es-Saam. Mwaka 1966 alipelekwa kusoma Teolojia katika Seminari Kuu
ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Tabora. Mwaka 1969 alihitimu masomo na
malezi ya seminari akapewa Ushemasi na mwaka huo huo tarehe 14 December
1969 akapewa sacramenti ya daraja la upadre na Mwadhama Cardinal Laurian
Rugambwa na akawa padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
UTUME WA UPADRE
Kwa muda wa miaka tisa alifanya
utume katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Alianza kama paroko
msaidizi nabaadaye paroko katika parokia kadhaa za Jimbo Kuu la Dar es
salaam. Tangu mwaka 1973 hadi 1976 aliteuliwa na Mwadhama Kardinali
Rugambwa kuwa Vikari wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es
salaam. Kutoka Dar Es Salaam alifanya utume pia katika Jimbo Kuu la
Arusha kwa muda mfupi kisha Mhashamu Askofu Denis wa Jimbo la Arusha
akamtuma Marekani kwa masomo ya Chuo Kikuu.
MASOMO YA CHUO KIKUU
Mwaka 1978 alienda Marekani
akasoma katika Chuo cha Majesuiti kilichoko
Berkeley, California, akatunukiwa Master Degree ya Teolojia mwaka 1982.
Alipenda bado kujiendeleza ndipo alipoenda katika Jiji la Washington DC
akasoma katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Amerika (Catholic
University of America) na akafuzu vizuri akatunukiwa Master of Arts
Degree in Religious Education mwaka 1987.
UTUME NCHINI MAREKANI
Padre Nyambo alikuwa padre wa
kwanza mwafrika kufanya kazi katika jimbo la St. Petersburg, Florida,
Amerika. Alianza kwa kufanya utume wakati wa kiangazi (Summer holidays)
katika parokia ya Mt. Joseph 1982 na Parokia ya Utatu Mtakatifu (Blessed
Trinity) mwaka 1986-1987.
Askofu wa jimbo la St. Petersburg
alifurahiwa na kuridhika na maisha na utendaji wa Padre Nyambo ndipo
akampa utume kamili kama wakili paroko katika parokia moja katika jiji
la Tampa, Florida mwaka 1988-1991. Wakati huo huo alikuwa Mkurugenzi wa
jimbo wa utume wa Wakatoliki Waamerika Weusi katika jimbo la St.
Petersburg.
Mwaka 1992-1993 alikuwa Paroko
Kiongozi wa parokia ya Mt. Peter Claver Tampa. Kwa kuwa alifanya utume
wake vizuri alipewa cheo cha Uparoko tangu mwaka 1993-1997.
Kwa muda wa miaka sita alikuwa
Paroko katika Parokia ya Mt. Joseph St Petersburg, yaani, tangu mwaka
1997 hadi 2003. Mwaka huo huo wa 2003 alikuwa Paroko wa Parokia ya
Watakatifu Wote (All Saints Parish) hadi mwaka 2013 alipostaafu
kisheria.
Pamoja na majukumu ya uparoko
na ya Kijimbo, Padre Nyambo alikuwa raisi wa utume wa Waamerika Weusi
Wakatoliki katika Mkoa wa Florida.
Tags
HABARI KITAIFA