Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amempongeza mshambuliaji wa timu ya
Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Mbwana Samatta kwa kufanikiwa kujiunga
na klabu ya Racing Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Ubeligiji.
Malinzi amempongeza Samatta kwa
kupata nafasi ya kucheza ligi kuu ya Ubeligiji baada ya kusaini mkataba
wa miaka mitatu na nusu kuichezea RC Genk inayoshika nafasi ya sita
kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.
Kufuatia kupata nafasi hiyo,
Malinzi amemtaka Samatta kujituma kwa nguvu zake zote na uwezo wake wote
ili kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika nyanja za
kimataifa na kwa sasa barani Ulaya.
Aidha Malinzi amewataka wachezaji
wengine kujituma na kutumia nafasi wanazozipata katika vilabu vyao kwa
kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuvuka kwenda kucheza soka la
kimataifa nchi za nje.
Tags
MICHEZO KITAIFA