Mkandarasi wa SynoHydo
Corporation Ltd akimkabidhi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya
Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa Km. 43.65 inaojengwa kwa kiwango cha lami
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akimuagiza Mkandarasi wa mradi wa
barabara ya Mayamaya-Mela kampuni ya China Henan International
Corporation Group Ltd (hayupo pichani) kuwapa mikataba bora ya kazi
wafanyakazi wanaojenga barabara hiyo (wanaomsikiliza).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mkandarasi wa
mradi wa barabara ya Mayamaya-Mela kampuni ya China Henan International
Corporation Group Ltd (pichani) kuwapa mikataba bora ya kazi wafanyakazi
wanaojenga barabara hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiagiza kuwekwa lami juu ya
Daraja la Kola Wilayani Kondoa mkoani Dodoma ili kuanza kupitika na
kupunguza usumbufu wa magari wakati wa mvua. (kushoto) ni Meneja ujenzi
wa barabara ya Mela-Bonga (Km.88.8) Eng. Stone Cheng na (Kulia) ni
Mhandisi Mshauri wa barabara hiyo.
Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu akitoa ufafanuzi kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu
kushoto) kuhusu hatua ya ujenzi iliyofikiwa katika barabara ya
Mela-Bonga (Km. 88.8) inayojengwa kwa kiwango cha lami, (Wa pili kulia)
ni Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Godfrey Kombe na (wa kwanza
kushoto) ni Eng. Deusdedit Kakoko kutoka TANROADS makao makuu.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Dodoma-Mayamaya Km. 43.65 ambao ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika kwa asilimia 80.
Kazi ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Mayamaya-Mela yenye urefu wa Km. 99.35 ukiendelea.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
…………………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewaagiza Makandarasi wa ujenzi wa
barabara kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi kwa kuzingatia haki,
usawa na taaluma ya mtu kama ilivyoelekezwa kwenye sheria ya ajira hapa
nchini ili kuwezesha kazi za ujenzi kukamilika kwa wakati.
Amesema hayo wilayani Chemba
Mkoani Dodoma wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Dodoma-Babati ambao
ujenzi wake umegawanywa katika sehemu tatu ambazo Dodoma-Mayamaya Km.
43.65, Mayamaya-Mela Km. 99.35 na Mela-Bonga Km. 88.8 ili kuharakisha
kasi ya kukamilika kwake.
“Hakikisheni leo hii mnawapa
mikataba halali kwa mujibu wa taaluma zao na inayozingatia sheria za
Tanzania ili kujega uhusiano mwema wa kiutendaji na hivyo kazi zenu
zitakuwa na tija na ubora unaokusudiwa”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amekagua madaraja
makubwa manne katika barabara hiyo ambayo ni Daraja la Kelema lenye
urefu wa mita 200, Msui lenye urefu wa mita 45, Kingali lenye urefu wa
mita 30, na Mela lenye urefu wa mita 30 na kuhimiza kasi ya ujenzi wa
madaraja hayo kabla ya mvua za masika.
Barabara ya Dodoma-Babati ni
sehemu ya Barabara Kuu ya Kaskazini (The Great North Road) inayoanzia
Cairo nchini Misri hadi Cape town Afrika Kusini.
“Barabara hii ni kiungo muhimu
cha miundombinu ya barabara za Tanzania kwani inaunganisha mikoa maarufu
ya kilimo ya nyanda za juu kusini, nyanda ya kati na nyanda ya
kaskazini na pia ni kiungo kikuu cha kwenda nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Eng. Deusdedit
Kakoko kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) makao makuu,
amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wamejipanga kuhakikisha barabara hiyo
ujenzi wake unakamilika kwa wakati ili kufungua fursa za kiuchumi na
kuunganisha kirahisi mkoa wa Dodoma, Manyara na Arusha.
“Mheshimiwa Waziri tutaendelea
kusimamia mradi huu umalizike kwa wakati na muda uliopangwa na
hatutaendelea kuvumilia wale wote wasioweza kumaliza mradi huu kwa
wakati”, amesisitiza Eng. Kakoko.
Waziri Mbarawa amezungumzia
umuhimu wa ubora wa barabara zinazojengwa na makandarasi wote nchini
kudumu kwa muda mrefu ili thamani ya fedha inayotumika kuwalipa iwiane
na huduma inayotolewa.
Hadi sasa sehemu ya barabara ya
Dodoma-Mayamaya (Km. 43.65), ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80
wakati barabara ya Mayamaya-Mela (Km. 99.35), ujenzi wake umekamilika
kwa asilimia 52.2 na ujenzi wa barabara Mela-Bonga (Km. 88.8),
umekamilika kwa asilimia 45.17 ambapo ujenzi wa barabara yote
Dodoma-Babati unatarajiwa kukamilika baadaye mwakani.
Tags
HABARI KITAIFA