TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KIKAO maalum cha Wakuu wa Nchi na
Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi
na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika)
kimeiagiza Serikali ya Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume
iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa nchini humo ifikapo
Februari Mosi, mwaka huu.
Agizo hilo lililotolewa kwa Waziri
Mkuu wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili katika kikao cha SADC Double
Troika kilichofanyika mapema wiki hii Gaberone, Botswana, chini ya
Mwenyekiti wake, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama ambaye pia
ni Rais wa nchi hiyo.
SADC Double Troika ni kikao maalum
cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi
wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics,
Defense and Security Cooperation) kilichofanyika kwenye kituo cha
mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Pamoja na kutaka Lesotho itangaze
matokeo ya tume hiyo, SADC Double Troika iliitaka nchi hiyo iandae
mchakato wa kueleza njia za utekelezaji wa mageuzi kama
yalivyopendekezwa kwenye ripoti ya tume hiyo ifikapo Agosti, mwaka
huu.
“Vilevile, nchi ya Lesotho
inatakiwa kuandaa mazingira wezeshi yatakayotoa nafasi kwa viongozi
wa upinzani na baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaoishi uhamishoni
ambao walikimbia machafuko, waweze kurejea nyumbani,” ilisema
sehemu ya taarifa iliyotolewa na sekretariati ya SADC siku moja baada
ya kikao hicho kumalizika.
Mkutano huo wa Botswana ulihudhuriwa
na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk.
John Pombe Magufuli; Rais wa Botswana, Luteni Jenerali Khama; Rais wa
Afrika Kusini, Bw. Jacob Zuma; Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto
Nyusi; Waziri Mkuu wa Swaziland, Dk. Barnabas Dlamini na Waziri wa
Mambo wa Nje wa Zimbabwe, Bw. Simbarashe Mumbengegwi ambaye
alimwakilisha Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.
SADC Double Troika ni mkutano
unaohusisha viongozi wakuu watatu wanaoongoza chombo cha ushirikiano
wa siasa, ulinzi na usalama na wengine watatu kutoka kwenye Mkutano
wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC. Hawa wanawakilisha mwenyekiti
aliyepo madarakani, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na mwenyekiti
ajaye ambaye huwa ni makamu mwenyekiti.
Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania
nchini Afrika Kusini, Balozi Radhia Msuya, chini ya muundo wa SADC,
kuna mambo makuu mawili; la kwanza likiwa ni utangamano wa kikanda
ambao unasimamiwa na mkutano wa wakuu wa nchi (SADC Summit) na la
pili ni la siasa, ulinzi na usalama ambalo linasimamiwa na chombo
maalum (SADC Organ).
Akifafanua zaidi, Balozi Msuya
alisema wajumbe wa mkutano wa SADC Organ ni Msumbiji (Mwenyekiti);
Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda wake) na Tanzania
inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo Agosti, 2016.
Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaunda SADC Summit.
Mapema, kikao hicho, kilipokea
taarifa ya msuluhishi wa SADC kwenye mgogoro wa Lesotho ambaye pia ni
Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Dk. Cyril Ramaphosa ambayo
iliainisha mambo kadhaa yakiwemo ya kikatiba na kiusalama ndani ya
nchi hiyo.
Dk. Ramaphosa alitakiwa kuhakikisha
kuwa mgogoro huo uliovihusisha vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi
ya Lesotho, unatatuliwa kwa njia ya mazungumzo kati ya wadau husika
ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo inarudi kwenye hali ya amani - kisiasa
na kiusalama.
Mgogoro wa Lesotho umehusisha kuuawa
kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Lesotho, Luteni. Jenerali
Maaparankoe Mahao, mnamo Juni 25, 2015. Pia baadhi ya wananchi
wanadaiwa kutiwa vizuizini na wengine kuwekwa ndani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 24, 2016.
Tags
HABARI KITAIFA