Naibu Waziri Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura akimsikiliza kiongozi wa msafara
wa Asasi za Kiraia toka mkoani Mtwara Dkt. Lillac Malumbo aliyesimama
wakati asasi hizo zilipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la
kubadilishana mawazo juu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati za
mkoa huo. (Picha na Benjamin Sawe-WHUSM)
Katibu wa msafara Bi. Rhobi Elias
akisoma risala kwa mgeni rasmi hayupo pichani kuhusiana na mila na
desturi hatarishi na zilizopitwa na wakati zinazoendelea kutumika katika
Mkoa wa Mtwara, mila hizo ni pamoja na kuwapeleka watoto wa kike kwenye
unyago wakiwa na umri mdogo, na ndoa za umri mdogo. (Picha na Benjamin
Sawe-WHUSM)
Katibu wa msafara Bi. Rhobi Elias
kushoto akimkabidhi risala Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Mh. Anastazia Wambura inayoelezea mila na desturi hatarishi na
zilizopitwa na wakati zinazoendelea kutumika katika Mkoa wa Mtwara, mila
hizo ni pamoja na kuwapeleka watoto wa kike kwenye unyago wakiwa na
umri mdogo, na ndoa za umri mdogo. (Picha na Benjamin Sawe-WHUSM)
……………………………………………………………………………………………..
Na Shamimu Nyaki MAELEZO.
Naibu Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia Wambura amezitaka jamii
kutoa elimu ya jando na unyago kwa kuzingatia umri na wakati sahihi wa
mafunzo hayo ili kuweza kuondoa tatizo la mimba na ndoa za utotoni.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es
Salaam wakati alipozungumza na Wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka
mkoani Mtwara wanaoshughulika na mapambano dhidi ya mimba na ndoa za
utotoni zinazosababishwa na utekelezaji wa wa mila na desturi hizo
mkoani Mtwara.
“Ni vizuri kuwafundisha watoto
wetu maadili mema wakiwa wadogo,lakini ni vizuri Kuandaa namna ya kutoa
elimu kwa kuzingatia umri na aina ya elimu ili kutoa taaluma hiyo kwa
watu sahihi na wakati unaofaa. Alisema Mhe.Anastazia.”
Mwenyekiti wa asasi hizo
Dkt.Lillac Malumbo akitoa taarifa ya jinsi wanavyoshughulikia tatizo
hilo amesema kuwa asasi zinatoa mafunzo mbalimbali kwa kwa wakufunzi
wa watoto wa kike ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni
linalosababishwa na utekelezaji wa mila mbalimbali mkoani Mtwara.
“Tunaamini kuwa jamii
ikielimishwa kuhusu madhara yatokanayo na baadhi ya mada
zinazotolewa katika mafunzo ya unyago na ambazo zinaleta ushawishi kwa
watoto wa kike kujiingiza katika zinaa, mimba na ndoa za utotoni tatizo
ili litaisha.Alisema Dkt. Lillac.”
Dkt Lillac ameongeza kuwa
kuweka ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na asasi hizo
kutamuwezesha mtoto wa kike kupata elimu, kuepuka magonjwa ya Zinaa
,kupunguza watoto yatima na watoto wa mtaani.
Hata hivyo mila hizi zimekuwa
zikiwanyima watoto wa kike haki ya kupata elimu kwa wakati, kusikilizwa,
kuendelezwa na kuwafanya kubaki tegemezi kwa muda wote.
Asasi hizi zinatoka katika
wilaya nne za mkoa wa Mtwara ambazo ni Tawaso Masasi,Msoapo Mtwara,Aware
Mtwara vijijini ,Chakumuma Masasi,Nyerere Tandahimba,Kimweso Mtwara
vijijini, pamoja na Children Youth Development Innitiatives (CYDI).
Tags
ELIMU