Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na mkandarasi Nyanza Road
Works anayejenga barabara ya Bulyamba-Kisolya yenye urefu wa Km 51. (Wa
kwanza kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bw. Joshua Mirumbe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Kisolya kuhusu ujenzi wa mradi wa barabara ya Bulyamba-Kisolya yenye
urefu wa Km 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa barabara ya
Bulyamba-Kisolya yenye urefu wa Km 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami
ambayo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda hadi Nansio Km 121.9.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Emmanuel Koroso (wa pili
kulia) wakati akikagua daraja la Kyarano linalounganisha barabara ya
Makutano-Nata- Mto wa Mbu yenye urefu wa Km 467.7.
Muonekano wa daraja la Kyarano
linalounganisha barabara ya Makutano-Nata- Mto wa Mbu yenye urefu wa Km
467.7 likiwa katika hatua za ujenzi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na watumishi wa sekta za
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani) kuhusu kufanya kazi kwa
umoja na kuongeza mapato katika sekta zao, mkoani Mara.
Meneja wa uwanja wa ndege wa
Musoma Bi. Bertha Bankwa akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa katika mkutano wa watumishi wa
sekta zilizo chini ya Wizara hiyo.
Daraja la reli linaloingia
baharini katika bandari ya Musoma kupokea na kupakia mizigo kwenye
melikwa ajili ya kuisafirisha katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya
nchi.
…………………………………………………………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka watendaji walio chini ya
Wizara yake kuongeza kasi ya kukusanya mapato ili kuwezesha malengo ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya
wananchi kufikiwa kwa wakati.
Akizungumza na watumishi wa sekta
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino mjini Musoma, Prof. Makame Mbarawa
amesema kufanya kazi kwa umoja, uadilifu, uwazi na ubunifu kutasababisha
kufikiwa kwa malengo hayo mapema.
“Kama mtu hawezi kufanya kazi kwa
kasi na kwa malengo yanayotekelezeka na kupimika atupishe kabla
hatujamuondoa, hatuta muonea mtu na hatutamvumilia mtu atakayeshindwa
kuendana na kasi yetu”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema Serikali
imetenga zaidi ya dola milioni 30 kwa ajili ya kukarabati uwanja wa
ndege wa Musoma na kununua magari ya kisasa ya zimamoto ili kurudisha
hadhi ya uwanja huo.
Aidha, amezitaka taasisi za
Serikali zinazodaiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Mara
kulipa madeni yao ili kuuwezesha wakala huo kufanya kazi kwa kasi na
kufikia malengo yaliyowekwa.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano-Nata-Mto wa Mbu yenye
urefu wa km 467.7 inayojengwa na makandarasi wazalendo kumi na kutaka
mkandarasi anayejenga kipande cha km50 kutoka Makutano hadi Sanzate
kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa haraka ikiwemo daraja la kyarano
ili kuiwezesha barabara hiyo kupitika wakati wote wa mwaka.
Amemwagiza Meneja Wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), mkoa Mara Eng. Emmanuel Koroso kuhakikisha
makandarasi wanaojenga barabara mkoani humo wanarejea kazini kwa kuwa
serikali imeanza kulipa madai yao.
Ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya
Butiama kutumia fedha zilizotumwa kutoka Mfuko wa Barabara (RFB)
kutumika kwa miradi iliyokusudiwa ili kuingunisha wilaya hiyo mpya na
wilaya nyingine mkoani Mara kwa barabara za lami.
Akiwa wilayani Bunda Prof.
Mbarawa amemtaka mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya
Buliamba-Kisolya Km 51 kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo kwa mujibu
wa mkataba kwani serikali imeshalipa fedha shilingi bilioni 8.5 kwa
ajili ya barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya
Nyamuswa-Bunda-Kisolya-Nansio yenye urefu wa Km 121.9.
Aidha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Prof. Mbarawa amewataka viongozi wa Wilaya za Magu,
Bunda na Musoma kufanya kampeni kubwa ya kuwaelimisha wananchi umuhimu
wa kulinda Miundombinu ya Barabara, Reli na Mkongo wa taifa wa
Mawasiliano ili isihujumiwe na kusababisha usumbufu kwa jamii na
kuisababishia serikali hasara.
Naye, Mbunge wa Mwibara Mhe.
Kangi Lugola amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kukamilika kwa
barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisolya hadi Nansio yenye urefu wa KM 121.9
itasaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Bunda na Ukerewe kwa kuwa eneo hilo
lina shughuli nyingi za uchumi zinazotokana na kilimo, ufugaji na uvuvi
wa Samaki.
Prof. Mbarawa amewataka
makandarasi wote nchini kuhakikisha wanawapa wafanyakazi wao mikataba
kulingana na sheria za nchi ili kuwezesha miradi ya barabara
inayoendelea kujengwa kukamilika kwa wakati na kuondokana na hujuma
zinazoweza kudhoofisha ujenzi wa barabara na miundombinu mingine.
“Lindeni miundombinu ili idumu
kwa muda mrefu, barabara, reli na mkongo wa taifa ni miongoni mwa
miundombinu inayojengwa kwa fedha nyingi na kuhujumiwa mara kwa mara
hivyo kuisababishia Serikali hasara”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa yupo kwenye
ziara ya kukagua Ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari na mkongo wa
taifa wa mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ametembelea
Wilaya za Magu, Bunda, Butiama na Musoma.
Tags
HABARI KITAIFA