Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inayo miongozo inayosimamia ufuatiliaji
wa magonjwa ya milipuko na miongozo hii imetolewa na kusambazwa katika
mikoa na wilaya zote nchini. Mwongozo huu unafuata utaratibu wa mfumo wa
ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated Disease
Surveillance and Response (IDSR)
Katika mwongozo huu, taarifa za
magonjwa ya milipuko kama Kipindupindu pindi yanapotokea hutolewa
taarifa mara moja kwa kutumia Ainisho sanifu yaani “Standard case
definition”. Aidha maainisho haya ya utambuzi wa ugonjwa yapo kwa ajili
ya jamii (Community case definition) na katika ngazi ya kituo cha Afya
(Health facility Case Definition).
Aidha utambuzi huu wa ainisho la
awali, huzingatia dalili za ugonjwa ili mgonjwa aweze kupatiwa huduma
wakati taratibu za vipimo zinapofanyika. Vipimo huchukuliwa kwa wagonjwa
10 wa awali wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa Kipindupindu, na iwapo mmoja
wao akithibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa basi uwepo wa mlipuko wa
ugonjwa husika hutangazwa.
Aidha kutokana na utaratibu huu,
ni wagonjwa wa mwanzo tu ndio watakaochukuliwa vipimo, na wengine
watakaoendelea kujitokeza huwa wanachukuliwa kuwa wana ugonjwa kwa kuwa
wana mahusiano na ushirikiano na wagonjwa waliokwisha thibitika
“epidemiological link”
Vipimo vya maabara huchukuliwa
tena kwa baadhi ya wagonjwa watakaoendelea kuugua ili kuweza kuangalia
mwenendo wa ugonjwa husika na pia kupima usikivu wa Dawa (Antimicrobial
Sensitivity Test).
Wizara inaendelea kusisitiza mambo manne muhimu:-
- Utoaji wa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu huzingatia Ainisho Sanifu yaani Standard case Definition bila ya kuwepo uthibitisho wa ugonjwa kimaabara
- Pindi ugonjwa ukisha thibitishwa kwa wagonjwa wa awali kumi (10) katika Mkoa/Wilaya/Halmashauri husika tayari mlipuko wa ugonjwa huu unathibitishwa na kutangazwa.
- Uthibishwaji wa ugonjwa kimaabara unafanyika tu kwa baadhi ya wagonjwa ili kuweza kuangalia mwenendo wa ugonjwa na pia kupima usikivu wa Dawa (Antimicrobial Sensitivity Test)
- Baadhi ya watu wenye ugonjwa wanaweza kupimwa na kuonekana kutokuwa na vimelea vya ugonjwa husika mfano kipindupindu. Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea kipimo kutoonyesha uwepo wa vimelea hivyo mojawapo ikiwemo wagonjwa kuanza kutumia dawa kabla ya kufika katika vituo vyetu vya tiba.
Kwa mfano katika Mkoa wa Dar es
salaam kwa siku kumi zilizopita kuanzia tarehe 7 hadi 16 Februari,
wagonjwa 16 wa kipindupindu (Temeke 12 na Ilala 4) walikidhi vigezo vya
ainisho sanifu na kupata matibabu katika kambi ya kipindupindu ya Temeke
kwa wagonjwa wa Temeke na Hospitali ya Amana kwa wagonjwa wa Ilala
hivyo kulazimu kutolewa taarifa kwa mujibu wa muongozo.
Hitimisho
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndio yenye dhamana ya kusimamia huduma za
afya kwa wananchi hivyo Wizara itaendelea kutoa taarifa za mara kwa
mara kwa wananchi kuhusu milipuko ya magonjwa ikiwamo kipindupindu.
Viongozi wa Mikoa na Wilaya wanao wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa
taarifa sahihi, mapema kwa kuzingatia miongozo na kwa wakati bila
kuficha pindi wanapopata wagonjwa wapya. Vilevile jamii isiwekewe
vikwazo vya faini au kunyanyapaliwa wapatapo ugonjwa huu kwani inaweza
kusababisha wananchi kuogopa kwenda katika vituo vya afya. Wakuu wa
Mikoa na Wilaya wawasiliane na Wizara iwapo kuna ufafanuzi wowote
unaohitajika kwa taarifa zinazotolewa.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
17 JANUARI 2015
Tags
AFYA