Kampuni kutoka
Falme za Kiarabu, Rental Solutions and Services LLC imeiburuza
mahakamani kampuni ya kufua umeme ya Symbion Tanzania Limited, ikidai
kulipwa Dola za Marekani 228,070,655.67 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 560 kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya kuzalishia umeme nchini.
Kesi hiyo Namba 234 ya mwaka 2016 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mdaiwa wa pili
katika shauri hilo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo
limeunganishwa katika kesi hiyo kama mdau mkuu kwenye sakata hilo ambapo
maamuzi yatakayotolewa na mahakama yanaweza kuiathiri.
Katika hati ya
madai, Kampuni ya Rental Solutions and Services inadai Symbion Dola za
Marekani 28,070,655.67 kama malimbikizo ya gharama za ukodishwaji wa
mitambo, ambayo hadi sasa Symbion imeshindwa kulipa na pia katika shauri
hilo Symbion itatakiwa kulipa Dola za Marekani milioni 200 ambazo ni
fidia kwa kampuni hiyo kula hasara kutokana na Symbion kuvunja masharti
ya mkataba na kuchelewesha au kushindwa kufanya malipo hayo.
Kwa mujibu wa
hati hiyo ya madai, fedha hizo zinatokana na kazi zilizofanywa na
kampuni hiyo ya Uarabuni ya kusambaza, kusimika na kuendesha mitambo ya
kuzalisha umeme ambayo ilikodishwa na Symbion kwa matumizi ya miradi
mbalimbali ya kuzalisha umeme kwa ajili ya Tanesco ili usambazwe kwenye
Gridi ya Taifa kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Rental
Solutions and Services pia katika kesi hiyo, inaiomba Mahakama kutamka
kuwa kushindwa kwa Symbion kulipa gharama hizo za ukodishaji kama
ilivyokubaliwa kwenye mkataba na pande zote mbili kumesababisha uvunjifu
wa mkataba na hivyo sio halali na haistahili kuendelea.
Inadaiwa kuwa
kati ya Septemba 2011 hadi Juni 2013, Rental Solutions and Services
iliingia mikataba mbalimbali na Symbion ambapo pale ilipohitajika
mikataba hiyo iliongezewa muda ili kukidhi mahitaji kwa mujibu wa
mikataba hiyo kwa lengo la kusambaza na kusimika mitambo ya umeme ili
kusambazwa kwenye Gridi ya Taifa.
Septemba 21,
2011 kampuni hiyo ya Uarabuni iliingia mkataba na Symbion kwa ajili ya
kusambaza na kusimika mitambo ya umeme katika Kituo cha Zuzu cha Tanesco
chenye nguvu ya kilovolti 33 kilichoko Dodoma yenye uwezo wa kuzalisha
megawati 50.
Katika mitambo
hiyo, pande husika zilikubaliana malipo ya Dola za Marekani 1,374,500
kwa mwezi kwa kipindi ambacho kingeishia miezi sita. Inadaiwa kuwa kwa
kipindi hicho, Symbion ingepaswa kulipa jumla ya Dola za Marekani
8,247,000.
Hati ya mdai
inaonesha kuwa mkataba kama huo uliingiwa na pande zote mbili Februari
12, 2012, kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 55 kwa kipindi
cha miezi 12 kwa gharama ya Dola za Marekani 1,666,000 kwa mwezi.
Mitambo hiyo
ipo katika vituo vya Arusha na Dodoma. Kwa mujibu wa hati ya madai,
kulikuwepo na ongezeko wa muda wa matumizi wa mitambo hiyo katika vituo
vya Dodoma na Arusha ambapo Rental Solutions and Services ilitimiza
matakwa yake kama ilivyo kwenye mikataba na iliwasilisha hati za malipo
kwa Symbion ili kukamilisha malipo ya kukodi kitambo hiyo kama
inavyotakiwa.
Tags
HABARI KITAIFA
