Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan amesema serikali haina nia ya kumwonea mtu,
inapochukua hatua ya kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Samia aliyasema
hayo juzi baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Morogoro, iliyosomwa na
Mkuu wa Mkoa huo, Dk Steven Kebwe akiwa katika ziara yake ya kikazi ya
siku tatu mkoani humo.
Alisema lengo
la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na
uwajibikaji serikalini, kama ilivyoangizwa katika Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mtasikia
katika serikali tunarekebisha, majipu yanatumbuliwa... kwa kweli hatuna
nia ya kumwonea mtu, tunarekebisha kama ilivyoagizwa katika Ilani yetu
ya Chama Cha Mapinduzi ili Watanzania wote wafaidi matunda ya nchi yao,” alisema Samia.
Alisema katika
marekebisho hayo, serikali imechukua hatua ya kukata mishahara ya walio
juu na kunyanyua ya walio chini waje juu kidogo na kwamba jitihada zote
hizo ni katika kufanya mambo yaende vizuri nchini.
“Tunapozungumzia
amani na utulivu ni pamoja na kuhakikisha kwamba walio chini wapo
vizuri, wasipokuwa vizuri hakuna amani na utulivu, kazi itawapata watu
wa kamati ya ulinzi na usalama, kuwatuliza kila siku na hawatatulizika
kwa sababu wana shida,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza: “Lakini
tukiwatuliza kwenye mambo yao wana maji, wana umeme, wana chakula,
mtoto anaenda shule vizuri, anapata afya, akienda zahanati dawa zipo,
watatulia tu.”
Alisema kwa
hivi sasa kuna tatizo la watumishi hewa na wengine wamediriki
kumdanganya mkuu wao wa kazi na hayo ndiyo mambo ambayo hayaleti picha
nzuri katika serikali.
Aliwataka wakuu
wa mikoa na wilaya nchini kuunga mkono jitihada hizo za serikali ili
kurejesha nidhamu na uwajibaikaji kwa watumishi wote. Wakati huo huo,
Makamu wa Rais ametembelea kiwanda cha kutengeneza nguo cha Mazava,
ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuzingatia masharti ya ajira na
wafanyakazi kuchapa kazi kwa bidii ili Taifa lipate kodi na wao wapate
mapato.
Akizungumza na
wafanyakazi, Samia aliuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa serikali
itazifanyia kazi changamoto za eneo na ukosefu wa ujuzi kwa kuwapeleka
vijana wengi kwenye vyuo vya elimu ya ufundi stadi (VETA) kujifunza
ushonaji.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo kwenye viwanda na kusisitiza
kwamba kupitia mpango wa EPZ, viwanda vingine vinatarajiwa kujengwa
mkoani humo, jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana.
Kiwanda hicho
ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2010 kina wafanyakazi zaidi ya 2,000
na kwamba asilimia 100 ya nguo zinazozalishwa kiwandani hapo, zinauzwa
nje ya nchi, ambapo soko kuu liko Marekani.
Tags
HABARI KITAIFA
