Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano(Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho
ameutaka uongozi wa Bandari unaosimamia Mitambo ya Kupimia Mafuta Nchini
(Flow Meter) iliyoko Kigamboni kutoa taarifa ya kuharibika kwa mitambo
hiyo ndani ya siku mbili.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Katibu Mkuu huyo alipofanya ziara ya kushtukiza katika mitambo
hiyo na kubaini upungufu katika vitendea kazi ikiwemo kamera ya
kufuatilia mwenendo bandarini hapo, “valvu, sloptank” na kuchelewashwa
kwa ujenzi wa kufunikwa kwa mitambo.
“Ifikapo Jumatatu nipatiwe
taarifa kuhusu matengenezo ya vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na
mnieleze lini ukarabati wake utakamilika” alisema Dkt. Chamuriho.
Aidha, aliongeza kuwa dhumuni la
Serikali ni kuhakikisha vifaa hivyo vinafanya kazi ili kulinda mapato
yatokanayo na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali
na hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.
Naye Meneja Mradi wa Mitambo ya
Kupimia Mafuta kutoka Mamlaka ya Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya
ameeleza kuwa uharibifu wa vifaa hivyo umesababishwa na mvua
zilizonyesha hivi karibuni na tayari vifaa hivyo vimeanza kufanyiwa
kukabarati.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Hebel Mhanga amesema ofisi yake
inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma sahihi kwa wateja wanaotumia
mitambo hiyo iliyopo bandarini hapo na Serikali inapata mapato
kulingana na huduma iliyotolewa.
Mradi wa Mitambo ya Kupimia
Mafuta nchini ipo katika majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo
tayari meli tatu zimefanyiwa majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja
ikiwa imefanyiwa vipimo.
Tags
HABARI KITAIFA