Watanzania wameombwa kutoa
maoni kuhusu njia zipi zitumike kutunza mazingira na kukomesha uvuvi
haramu wilayani Temeke katika tamasha la mazingira litakalofanyika Mei
27, 2016 kwenye fukwe za Sunrise – Kigamboni.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu wa
CFMA (Collaborative Fisheries Management Area) Godfrey Maduhu alisema
wao wakiwa wadau wa mazingira wameandaa tamasha lenye lengo la kupiga
vita uvuvi haramu na utunzaji wa mazingira.
Maduhu alitoa kauli hiyo wakati
wa mkutano huo, ambao ulishirikisha Mtandao wa Usimamizi Shirikishi wa
Kusimamia Rasimali za Pwani na Bahari, Balozi wa kujitolea na wadau
sekta ya mazingira(WWF).
“Tunapenda kuujulisha umma
kuhusiana na tamasha litakalohusisha wadau mbalimbali wa mazingira,
litakalokwenda kwa jina la ‘kwa heri Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, karibu
Dkt. John Pombe Magufuli,’ lenye lengo la kupiga vita masuala ya uvuvi
haramu na kuhamasisha jamii juu ya usimamizi na utunzaji wa mazingira,”
alisema Maduhu.
Aidha, Maduhu alisema kwamba
lengo la tamasha hilo ni kupanga mikakati juu ya utunzaji na
uendelezwaji mzuri wa mazingira na kusikia kauli kutoka viongozi ngazi
ya juu hususani kuhusiana na changamoto katika suala la utunzaji wa
mazingira.
Maduhu alisema kwamba kama
hakutakuwepo na mikakati ya kushughulikia changamoto juu ya uvuvi
haramu, Serikali itapoteza mapato mengi kwa kupoteza wateja kutokana na
milipuko ya mara kwa mara katika fukwe za bahari na kupelekea watalii
kuhofia maisha yao.
Alitaja changamoto nyingine
kuwa ni kupungua kwa kipato cha wananchi na Taifa kutokana na kupungua
kwa samaki katika Bahari ya Hindi na ongezeko la wagonjwa wa kansa
kutokana na kula samaki waliouliwa kwa kutumia baruti.
Kwa upande wake, Balozi wa
mazingira wa kujitolea Omary Kombe alisema kuwa, mazingira bado machafu
hivyo ameitaka Serikali kuendelea kukazia suala la usafi ikiwezekana
hata kwa kuweka faini kwa mtu atakayeonekana kuchafua mazingira.
Tamasha hilo litahusisha
viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya Serikali za Mtaa, Wilaya, Mkoa na
Taifa.Pia kutakuwa na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi juu ya
njia gani zitumike kuboresha utunzaji mazingira na kukomesha uvuvi
haramu.
Tags
HABARI KITAIFA