Wizara ya M aliasili
na Utalii imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika
maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika kuwa na Mamba au Viboko na
kuwasilisha taarifa za matukio haraka kwa Viongozi wa Vijiji husika na
Maafisa Wanyamapori walio karibu ili kumbukumbu za matukio na hatua
stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
Kauli hiyo imetolewa
leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe.
Ramo Makani wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini, Mhe. Esta
Bulaya ambaye alitaka kujua jinsi gani Serikali imejipanga katika kuokoa
maisha ya Wananchi kutokana na hatari kubwa ya mamba hao.
Mhe. Makani amesema
kwamba baadhi ya Vijiji vilivyotajwa na Mhe. Mbunge Esta Bulaya
vinapatikana na Ziwa Viktoria na mazingira hayo yanasababisha kuwepo na
mwingiliano wa shughuli za kibinadamu na makazi ya wanyamapori kama vile
mamba pamoja na viboko ambayo yanaweza kusababisha matukio ya wananchi
kuuawa na kujeruhiwa na wanayamapori hao.
“Wizara yangu
imepokea taarifa zilizowasilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda
ambazo zinaendelea kuhakikiwa, kwamba katika kijiji cha Guta jumla ya
wananchi wanne waliuawa na wengine tisa kujeruhiwa na mamba katika
kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015”, alisema Mhe. Makani.
Aliendelea kusema
kwamba katika kipindi hicho, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na
kupokelewa kuhusu matukio katika vijiji vya Tairo, Nyamtwali na Njabeu.
Alifafanua kuwa,
Kifungu cha 69 cha Sheria ya Kuhifafhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009,
kimempa mamlaka Mkurugenzi wa Wanyamapori kukasimu majukumu ya
kushughulikia masuala ya Wanyamapori wakali na waharibifu kwa Afisa
aliyeidhinishwa.
Aidha, Sheria
imeainisha utaratibu wa kutoa taarifa za matukio kuanzia kwa Mtendaji wa
kijiji, Maafisa Wanyamapori walioko karibu hadi Wizarani kwa hatua
zaidi.
“Ili kuokoa maisha ya
wananchi kutokana na hatari ya mamba na viboko katika vijiji
vilivyotajwa, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
(TAWIRI) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itafanya
tathmini ya ongezeko la mamba, na iwapo itadhihirika kuwa idai yao ni
kubwa kuliko viwango vinavyokubalika hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa
ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwavuna wanyama hao”, alisema Mhe.
Makani.
Aliongeza kuwa
utaratibu huo utatumika katika maeneo yote yenye uhatarishi wa mamba na
viboko. Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi, jinsi ya
kujilinda na kujiepusha na wanayamapori wakali na waharibifu wakiwemo
mamba pamoja na taratibu za kuwasilisha madai ya malipo ya kifuta jasho
na machozi kwa wale watakaoathirika.
“Pamoja na jitihada
hizo za Serikali, Wizara inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua
tahadahari katika maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika kuwa na
Mamba au Viboko na kuwasilisha taarifa za matukio hayo haraka kwa
Viongozi wa Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori”, alisisitiza Mhe.
Makani.
Tags
HABARI KITAIFA