Balozi wa kujitolea wa
mazingira, Omary Kombe ameiomba Serikali kuwatambua watu wanaobadilisha
taka kuwa bidhaa kwa kuendeleza taaluma hiyo ili kuinua uchumi na
kuondokana na tatizo la uchafu nchini.
Akiongea na waandishi wa habari
Mei 18, 2016 jijini Dar es Salaam, Kombe alisema kwamba kwa
kuwatambua watu hao, tatizo la taka litakwisha kwa kiwango kikubwa
nchini hasa katika jiji la Dar es Salaam.
“Wapo watu ambao mara nyingi
tunawaona kwenye maonyesho mbalimbali kama vile sabasaba ambao wanauwezo
wa kubadili taka kuwa bidhaa za majumbani kwa mfano, mkaa, mapambo na
bidhaa nyingine, ni vizuri Serikali ikawatumia watu hao kuondokana na
tatizo la taka nchini,” alisema Kombe.
Aliongeza kwamba mazingira bado
ni machafu licha ya serikali ya awamu ya tano kuweka mkazo katika
suala zima la usafi kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa ili kukabiliana
na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Kombe alisema kwamba, tatizo
hilo la uchafu litatatuliwa kama watu wenye uwezo wa kubadilisha taka
kuwa bidhaa watatambuliwa na kufanya kazi hiyo kuwa rasmi.
Aidha alisema kuwa, kwa
kubadilisha taka kuwa bidhaa kutapunguza kiwango cha taka nchini,
kuongeza ajira pamoja na kuipunguzia Serikali mzigo wa kutenga maeneo
kwa ajili ya kuhifadhia taka kila mara.
Usafi ni kauli mbiu
ambayo imeshika kasi awamu hii ya tano ambapo katika sherehe za Uhuru
(Tisa Desemba) Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwataka watanzania wote
kushiriki usafi maeneo yanayowazunguka na vituo vya jamii kama
hospitali, zahanati na vituo vya afya.
Tags
BIASHARA