…………………………………………………………………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi
Hainan International Limited anayejenga Daraja la mto Sibiti ambalo
linaunganisha mkoa wa Singida na Simiyu kuendelea na ujenzi wake.
Amesema hayo mara baada
ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo na kuwahakikishia
wananchi kuwa daraja hilo litakamilika katika kipindi cha hivi karibuni
baada ya Serikali kuanza kumlipa mkandarasi huyo.
“Tumeanza kumlipa
mkandarasi fedha hivyo tunawahakikishia kwamba katika kipindi kifupi
kijacho litakamilika ili kufungua shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa
Wilaya ya Mkalama na Meatu” , amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Waziri huyo wa
Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano amekemea tabia ya baadhi ya wananchi
kutoza ushuru katika mto huo na kusisitiza kwamba tabia hiyo iachwe mara
moja na atakayefanya hivyo anakiuka sheria na hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake.
“Wananchi wanatakiwa
kupita hapa bila ya kulipa gharama yoyote katika mto huu, nimemuagiza
Mkuu wa Wilaya na Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida waboreshe eneo la
kuvukia ili wakati ujenzi unaendelea huduma za kuvuka ziendelee kama
kawaida”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo
amemhakikishia waziri kuwa ujenzi wa Daraja la mto sibiti pia utahusisha
barabara ya maingilio yenye urefu wa kilomita 25 inayounganisha wilaya
ya Mkalama na Meatu.
“Ujenzi wa barabara za
maingilio unahusisha makalvati makubwa 10 na madogo 55 ili kuruhusu maji
kupita kwa kasi na hivyo kudhibiti mafuriko”, amefafanua Eng. Kapongo.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Mkalama Bw. Christopher Ngubiagai amemshukuru Waziri Prof.
Mbarawa kwa jitihada zake za kutaka kuunganisha wilaya yake na Meatu
kwani kukamilika kwa daraja hilo kutaimarisha fursa za usafirishaji wa
mazao na huduma za usafiri katika Wilaya hizo.
Zaidi ya shilingi
bilioni 18.2 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Daraja la mto Sibiti
lenye urefu wa mita 82 na upana wa mita 10.5 ambapo tayari Serikali
imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 4 mpaka sasa.
Katika hatua nyingine
Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa nyumba za viongozi wa Wilaya ya Mkalama
na jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwataka makandarasi
wanaoendelea na ujenzi wa miradi hiyo kuongeza kasi na kutumia fedha
wanazopata kujenga jengo moja moja kwa awamu ili kupunguza changamoto
ya makazi na ofisi Wilayani humo badala ya utaratibu wa sasa wa kujenga
majengo yote kwa pamoja.
.”Msisubiri mpate
fedha zote kwa nyumba zote, kamilisheni ujenzi wa nyumba moja moja
kadri mnavyopata fedha ili kupunguza changamoto za makazi na ofisi”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa yuko
katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne mkoani Singida ya kukagua
miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, nyumba na Mawasiliano.
Tags
HABARI KITAIFA