Pia amewaagiza watendaji wote wa
Serikali, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Maofisa Elimu,
Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa
Wilaya na Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha michango hiyo inayotolewa inawafikia walengwa.
Aidha, amezitaka wilaya zote
nchini zianzishe mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba upungufu wa
madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao na kwamba utendaji wa
viongozi wa elimu na Serikali katika ngazi mbalimbali utapimwa kutokana
na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema
hayo leo (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati wa matembezi ya hisani ya
kukusanya fedha za kununulia madawati kama sehemu ya maadhimisho ya
miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Katika maadhimisho hayo
yaliyoanzia BOT hadi viwanjja vya Mnazi Mmoja, Gavana wa BOT, Profesa
Benno Ndulu alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya shilingi milioni 263
zilizochangwa na benki hiyo pamoja na watumishi wake kama mchango wao
kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
Waziri Mkuu aliwapongeza
watumishi wa BOT kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto
hiyo ambapo alitoa wito kwa taasisi zote katika sekta ya umma na binafsi
pamoja na watu binafsi kuchangia uboreshaji wa elimu nchini kama sehemu
ya “Majukumu ya Taasisi kwa Jamii” (Corporate Social Responsibility).
Amesema kuwa na elimu bora, siyo
tu faida kwa Taifa, bali kwa waajiri pia, kwani itahakikisha kwamba
taasisi za umma na binafsi zinapata wafanyakazi ambao wameiva na wenye
weledi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji katika taasisi
hizo.
“Nitoe wito pia kwa wanafunzi
wote ambao watafaidika na kuboreshwa kwa mazingira ya kusomea, ikiwemo
kupewa madawati na mahitaji mengine, kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa
faida yao na Taifa kwa ujumla na kwa kufanya hivyo, wanafunzi watakuwa
wanaenzi jitihada za Serikali, taasisi za umma, taasisi binafsi na watu
binafsi katika kuboresha elimu nchini,” amesema.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
imeazimia kupambana na changamoto za sekta ya elimu na kwamba tangu
Uhuru, Serikali za Awamu zote zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali
katika kuboresha elimu kwa wananchi wake.
Tags
ELIMU