BANDA MEDIA BLOG

MIAKA 23, FRANK DOMAYO ANAPASWA KUFANYA HAYA ILI KUOKOA KIPAJI CHAKE


Frank Domayo, kiungo wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' na Azam FC
Na Baraka Mbolembole
FRANK DOMAYO bado yupo kwenxe orodha ya wachezaji bora wa nafasi ya kiungo wa kati katika ligi kuu ya Tanzania Bara, kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 23 usisahau kuwa ni wakati wa kuingia kwenye kipindi muhimu cha maisha ya soka lake.

Lakini badala yake, Domayo amekuwa akisugua benchi katika timu ya Azam FC kwa misimu miwili sasa huku wakati mwingine  akilazimika kucheza katika nafasi ambazo hana uzoefu nazo. Domayo ni kiungo wa kati mwenye kupiga pasi timilifu za mbali lakini mbele ya Himid Mao, Kipre Bolou, Salum Abubakar, Jean Mugiraneza ameshindwa kutamba.
Na miaka yake miwili katika timu ya Azam FC imekwisha tofauti na matarajio si yake tu bali hata kwa Azam wenyewe na wadau wa kandanda nchini. Domayo alicheza kwa msimu mmoja katika timu ya JKT Ruvu ya Pwani akiwa na miaka 18 msimu wa 2011/12.
Alisajiliwa Yanga mwezi Julai, 2012 na katika klabu hiyo alifanikiwa kuwa kipenzi cha makocha na mashabiki wa timu hiyo kutokana na kipaji chake kilichoambatana na pasi za uhakika.
Yanga haikutaka kumuacha Domayo lakini mchezaji huyo aliamua kutoongeza mkataba mpya mara baada ya ule wa awali kumalizika. Domayo aliichagua Azam FC katikati ya mwaka 2014.
Wengi walisema kwamba usajili huo ulisukumwa zaidi na mambo ya kimaslahi kwani kiungo huyo wa zamani wa timu ya Taifa alivuta zaidi ya milioni 90 katika mkataba wa miaka miwili katika timu hiyo ya Chamanzi.
Kwa mara ya kwanza Domayo alipojumuishwa katika timu ya Taifa Stars mwanzoni mwa mwaka 2012 na kuanza kucheza michezo ya kimataifa, alitajwa kama kiungo bora zaidi wa kati aliyekuwa akichipukia, lakini kwa sasa mambo yamekuwa tofauti kabisa.
Frank amepungua uwezo wake wa kawaida kiuchezaji tangu alipotoka Yanga na kujiunga na Azam. Lakini naamini katika umri wake wa miaka 23, Domayo bado ana safari ndefu ya mafanikio.
Anapaswa kuchagua timu mpya ambayo atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kufufua uwezo wake. Azam imeonekana haitamuongeza mkataba mchezaji huyo ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Akiweka kando suala ya maslahi na kujiunga na timu kama Mbeya City FC, Mwadui FC, Mtibwa Sugar bila shaka kijana huyo atarejea katika ubora wake. Inasikitisha kuona kiwango cha chini kutoka kwa Domayo hivi sasa, wakati mchezaji huyo ni mdogo kwa Thaban Kamusoko na Justice Majabvi ambao walifanya vizuri katika VPL msimu uliopita wakiwa na timu za Yanga SC na Simba SC.
Sawa kuna baadhi ya mechi aliweza kuonesha uwezo, ikiwemo kufunga baadhi ya magoli ya kuvutia, lakini bado inaonekana nafasi ya mchezaji huyo katika kikosi cha kwanza isingekuwepo. Ni wazi jambo hilo lilimkwanza na hakupendezwa nalo-kutokuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza katika timu kama Azam FC.
Kitu ambacho sasa kimemfanya asitambulike kama kiungo bora wa kati raia wa Tanzania katika VPL. Domayo wa msimu uliopita alikuwa akipoteza sana mipira, na kwa jinsi mchezaji huyo alivyokuwa akicheza JKT Ruvu na Yanga nakiona ni kitu tofauti na alivyozoeleka mchezaji huyo alipoanza kung’ara.
Ni kweli baada ya misimu mitano tu VPL, Domayo anajiona yupo njia panda, na kuibua maswali kwa mashabiki ni namna gani mchezaji huyo anaweza kuibuka. Jibu rahisi kwa Domayo ni kutafuta timu yenye ushindani katika ligi ambayo atapambana kurejea katika ubora wake.
Kutoka JKT hadi Yanga akiwa U20 yalikuwa ni mafanikio makubwa sana, ukitazama na mchango wake katika timu hiyo ya Twiga na Jangwani ni wazi Domayo alikuwa ni miongoni mwa mastaa makinda waliofanikiwa.
Kujiunga Azam FC akitokea kikosi cha kwanza cha Yanga ilikuwa sawa tu kwa maana alipata pesa na alijiunga katika timu iliyokuwa na ubingwa wa VPL. Na sasa anapaswa kufanya chaguo lingine sahihi kwa kujiunga na timu ambayo itampa zaidi nafasi ya kucheza na si pesa pekee.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG