Dar es Salaam
Serikali kupitia Wakala wa
Misitu Tanzania imewataka watendaji kuanzia ngazi ya kijiji kupanda miti
takribani kiasi cha hekta 185,000 za miti kwa mwaka ili kukabiliana na
changamoto ya upungufu wa misitu nchini.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi
wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali, Wakala wa Misitu Tanzania Bw.
Mohamed Kilongo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
utaratibu wa uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.
Alisema kuwa ifikapo mwaka 2030
upungufu wa misitu utakuwepo endapo serikali haitatekeleza mkakati wa
upandaji wa miti, hivyo kuwataka watendaji hao kutekeleza mkakati wa
upandaji wa miti uliowekwa na Wakala wa misitu.
“Tumekubaliana katika mkakati wa
kitaifa kuwa kila wilaya kupanda miti Milioni 1.5 kila mwaka ili
kuondokana na tatizo la upungufu wa misitu nchini ifikapo mwaka 2030”
Alifafanua Bw. Kilongo.
Aliongeza kuwa upungufu huo
unatokana na kichocheo cha uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya
hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za taifa hivyo
kuwataka wavunaji wa mazao ya misitu kufuata sheria na taratibu
zilizopo.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa huduma za Misitu Prof. Dos Santos Silayo alisema kuwa endapo
wavunaji na wasafirishaji wa mazao ya misitu watatumia taratibu za
uvunaji na usafirishaji wa mazao hayo itasaidia kuongeza pato la taifa.
“Vyombo vyote vitakavyohusika na
kusafirisha mazao ya misitu ni lazima viwe wazi ili ukaguzi ufanyike
kwa urahisi na ufanisi ambapo kila atakayesafirisha mazao ya misitu
anapaswa kusimama kwenye kizuia kwa ajili ya ukaguzi”alisema Prof
Silayo.
Mbali na hayo Wakala wa Misitu
Tanzania imejipanga kutoa mafunzo maalumu kwa wananchi juu ya uhifadhi,
uvunaji,usafirishaji, usimamizi na utunzaji wa mazao ya Misitu.
Tags
HABARI KITAIFA