Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida John Mwombeki akisoma taarifa
ya hali ya afya Mkoa wa Singida wakati wa uzinduzi wa huduma tembezi za
kibingwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe
akihutubiwa wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma tembezi za madaktari
bingwa Mkoani Singida.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Meno akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi za kibingwa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho akimhudumia mteja siku ya kwanza ya huduma tembezi za kibingwa.
……………………………………………………………………………
……………………………………………………………………………
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi
Mathew J. Mtigumwe amezindua huduma tembezi za madaktari bingwa humo na
kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za kibingwa.
Huduma zilizozinduliwa Wilayani
Iramba katika hospitali ya Kiomboi zitahusisha huduma za za upasuaji,
meno, macho, upasuaji wa mifupa, huduma za kibingwa za magonjwa ya
watoto, wanawake na huduma za mionzi.
Mhandisi Mtigumwe amesema
matarajio ya mkoa huo ni kuwa huduma tembezi za kibingwa zitasaidia
kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali kabla hayajafikia hatua ya usugu
na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa.
“Huduma tembezi za kibingwa
zitawasaidia wananchi kutambua uwepo wa huduma za kibingwa katika mkoa
wa singida na kupata matibabu kwa gharama nafuu” alisema Mhandisi
Mtigumwe.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.
John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya Mkoa wa Singida amesema
wazo la kuanzisha huduma tembezi za kibingwa limetokana na idadi kubwa
ya operesheni zilizofanyika kwa mwaka 2015/2016 na pia mkutano wa wadau
wa afya mkoani hapa kuafiki wazo la kuanzisha huduma hiyo.
“Kwa kipindi cha mwaka
2015/2016 jumla ya operesheni kubwa na ndogo 4,836 zimefanyika katika
hospitali mbalimbali mkoani hapa, aidha Idara ya macho katika hospitali
ya Mkoa imefanya jumla ya operesheni kubwa na ndogo 2,020” ameongeza
Dkt. Mwombeki.
Dkt. Mwombeki amesema uwepo wa
madaktari bingwa 11 mkoani Singida pia umekuwa chachu ya utekelezaji wa
huduma hiyo huku Mkoa ukifanya jitihada za kuazima madaktari wengine
katika mikoa jirani ya Dodoma na Manyara.
Baadhi ya wagonjwa waliohudhuria
katika siku ya kwanza ya zoezi hilo huku huduma hiyo ikitarajiwa
kufanyika kwa muda wa siku tano wilayani hapo wameeleza shauku na furaha
yao ya kusogezewa huduma za kibingwa katika halmashauri zao.
“Nilikuwa naumwa jino ambalo
limeota vibaya, niliambiwa nitaweza kufanyiwa operesheni katika
hospitali kubwa kama Muhimbili lakini hawa madaktari wametusaidia ,
nimepata huduma haraka na kwa gharama nafuu, nawasihi wenzangu waje kwa
wingi” amesema Bi Neema Josseph Mkazi wa Kijiji cha Kizaga Wilayani
Iramba.
Naye Mzazi wa mtoto Jonas
Masaka amesema huduma za kibingwa zitamsaidia mtoto wake mwenye matatizo
ya macho na hiyo kumpunguzia gharama ya kumpeleke katika hospitali
kubwa kutibu tatizo la macho linalomsababisha mtoto huyo kushindwa
kusoma vizuri.
Huduma ya tembezi za kibingwa
Mkoani Singida zitafanyika katika Wilaya zote tano za Mkoa nwa Singida
na hvyo kupunguza wagonjwa wa rufaa watakaopelekwa hospitali za Bugando,
KCMC na Muhimbili.
Tags
AFYA