BANDA MEDIA BLOG

Jicho la 3: ‘Hans anaponikosoa mapema, lakini maamuzi yake mengine yanashangaza sana…’


dsc_0020
Na Baraka Mbolembole
Uaminifu si usaliti, bali ni kumtii mtu na kumkubali. Mwaka mmoja uliopita sikuingia katika mkumbo wa kulaumu usajili wa mlinzi wa kati, Mtogo, Vicent Bossou.
Niliamini ‘ukuta’ wa Yanga SC ulikuwa na nyufa nyingi za kuzibwa. Mechi yake ya kwanza, Yanga 4-1 Toto Africans nikaandika ‘Bossou hakunaga,’ nilimsifia sana, mwishowe baadhi ya watu wakasema amecheza dhidi ya timu dhaifu.
Kumbe nilikuwa na maana nyingine kabisa na anachoendelea kufanya mlinzi huyo wa Togo klabuni Yanga ni hadithi nzuri ya kujifunza.

Sijui kwanini niliandika, ‘Hans katika sajili 3 za kishabiki, Dante wa nini Yanga?’
Je, nilikosea kumkosoa kuhusu usajili wa mlinzi huyo wa kati wa timu ya Taifa ya Tanzania? Nilikosea kuuponda usajili wa mlinda mlango, Beno Kakolanya? Sijawahi kuwa na imani na usajili ghali zaidi Tanzania uliomleta Mzambia, Obrey Chirwa kwa kitita cha zaidi ya milioni 200! Sasa nina sababu ya kuukubali ujio wa Dante.
DANTE
Licha ya kimo chake cha wastani, Dante amekuwa akiruka juu na kuicheza mipira mingi ambayo ilipaswa kuwafikia wapinzani wake. Hans amekuwa akimsifia mlinzi huyo kijana na hajaishia kumsifia tu bali kumpa mbinu na nafasi ya kucheza katika kikosi chake cha kwanza.
Wakati alipomsaini Bossou mwaka mmoja uliopita niliamini Yanga inakosa mtu mtulivu katika ngome ya kati. Nahodha, Nadir Haroub na patna wake wa muda mrefu, Kelvin Yondan walikuwa na makosa ya mara kwa mara katika kujipanga, kuanzisha mashambulizi na jinsi ya kujihami.
Hawa si watulivu ndiyo maana alipoanza kucheza Bossou ngome ikaonekana hairuhusu magoli mengi kwa maana mlinzi huyo wa timu ya Taifa ya Togo ni mtulivu, kiongozi ambaye anaweza kujiongoza na kuwapanga wenzake.
Mfano, Kelvin na Nadir huwezi kuwaona wakijiamini kwa kuutoa mpira nje ya uwanja ili iwe kona itakayopigwa upande wao. Bossou anaweza kutazama mazingira ya kuupeleka mpira pindi anapokuwa nao baada ya shambulizi lakini akiona uwezekano mdogo wa mpira kubaki kule anapotaka uende uchukua uamuzi wa kuutoa ili kona na muda huo wa kupigwa kona huipanga beki yake.
Bossou anaweza kuzima presha ya mashambulizi ya timu pinzani kutokana na utulivu wake. Aliposajiliwa Dante nikahoji mlinzi huyo alikuwa wa nini katika safu ya ulinzi ya kati ambayo tayari walikuwapo, Bossou, Kelvin na Nadir huku pia Mnyarwanda, Mbuyu Twite akiwa na uwezo wa kucheza katika nafasi hiyo.
Wengi wakati ule nilipoandika walizungumzia kuhusu umri wa Kelvin, Nadir na Bossou ila sasa naanza kuona sababu ya ziada zaidi na bora ambayo pengine ndiyo ilipelekea Hans akapendekeza usajili wa mchezaji huyo aliyekuwa na miaka miwili ya kupenda katika kikosi cha Mtibwa Sugar.
Bila shaka, Hans alimtaka mlinzi ambaye atavuruga mipira yote ya juu itakayoelekezwa golini kwa Yanga na Dante anafanya hivyo bila kuchoka.
Nilikuwa na sababu za kuhoji usajili wake mwezi Juni lakini miezi mitatu baadae nakubaliana na uamuzi wa mlinzi huyo kusajiliwa Yanga kwa maana hadi sasa ameleta kitu tofauti katika uchezaji wa safu ya ulinzi ya Yanga na timu kiujumla.
Huyu ndiye mchezaji wangu bora hadi sasa katika michezo mitatu ya Yanga. Anacheza vyema akiwa na Bossou, Nadir au Kelvin kwa maana hiyo anauwezo mkubwa wa kuusoma mchezo na wachezaji wenzake.
CHIRWA 
Ni kweli huyu Mzambia anapaswa kuendelea kupewa muda? Mechi zake tatu za Caf Confederation Cup 2016 hatua ya makundi zilikuwa nzito kwake na kiwango chake vs Ndanda FC wiki-jana katika VPL kiliendelea kunifanya niamini Hans hakufanya uamuzi mzuri kumsaini mshambulizi huyu kutoka FC Platnum ya Zimbabwe.
Urafiki wake na Donald Ngoma umechangia sana ujio wa Chirwa lakini magoli ya wazi aliyokosa katika game hiyo ya suluhu-tasa siku ya Jumatano iliyopita pale Nangwanda Stadium, Mtwara na kiwango kingine cha kawaida vs Majimaji FC siku ya Jumamosi iliyopita kinaendelea kuacha maswali kama kweli mchezaji huyo ana thamani ya zaidi ya milioni 200.
Huyu Mzambia anaweza kufunga siku za mbele lakini game zake tano za mwanzo klabuni Yanga zinaashilia ni usajili mwingine usio na faida kwa Yanga, bila shaka huyu Chirwa ana mzigo mzito anaopaswa kuufikisha mahali. Mechi 5 bila goli! Kwa straika ni kufeli!
Kwanini Hans alipendekeza sajili hii na kuifanya iwe ghali kuliko zote katika mpira wa Tanzania? Wewe bado unampa muda Chirwa? Unafanya makosa.
Ningekuwa_katika nafasi ya Hans van der Pluijm, Obrey Chirwa ningependekeza aende Toto Africans kwa mkopo halafu nawasaini tena Andrey Coutinho na ‘mchezaji wa Yanga,’ Mrisho Ngassa katika dirishb dogo lijalo.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG