Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora
akizungumza wakati akifunga warsha ya wadau na wataalamu kutoka Shirika
la Mawasiliano la Jumuiya ya Madola (hawapo pichani) kuhusu uandaaji wa
Mkakati wa Kitaifa wa Usalama katika Mitandao nchini.
Afisa Mwandamizi wa ufundi na
ushauri wa Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya madola Bw. Fargani
Tambeayuk akitoa shukurani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano pamoja na wadau wengine baada ya kumalizika kwa warsha ya
uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama katika Mitandao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
TEHAMA wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Shabani Pazi
akizungumza wakati akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi ,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora
(hayupo pichani) wakati wa kufunga Semina ya Uuandaaji wa Mkakati wa
Kitaifa wa Usalama katika Mitandao leo. Jijini Dar es Salaam.
Wadau wa Sekta ya Mawasiliano
wanaoandaa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama kwenye Mtandao wakimsikiliza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora (hayupo pichani) wakati wa kufunga
warsha ya wadau na wataalamu kutoka Shirika la Mawasiliano la Jumuiya
ya Madola wanaoandaa mkakati huo.
…………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano ( Sekta ya Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora
ametoa wito kwa vyuo vyote nchini kuanzisha mitaala inayohusu usalama wa
mitandao ya mawasiliano ili kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao
hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar
es Salaam na Katibu Mkuu huyo alipokuwa akifunga warsha ya siku ya wadau
na wataalamu kutoka Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya Madola
iliyohusu Uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Usalama wa Mitandao
iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania.
Prof. Kamuzora amesema kuwa moja
ya vitu vilivyoelezewa katika Sera ya Tehama iliyotolewa mwezi Mei mwaka
huu ni kuhakikisha mitandao ya mawasiliano inakuwa salama hivyo kila
mwananchi anawajibu wa kulinda mitandao hiyo.
“Suala la usalama wa mitandao ya
mawasiliano linapelekea kuwepo kwa fursa nyingi za ajira hivyo, napenda
kutoa wito kwa vyuo mbalimbali nchini kuanzisha mitaala mipya
itakayohusu masuala haya kwa sababu watu watatakiwa wajikite kwenye
masomo yanayohusiana na mitandao”, alisema Prof.Kamuzora.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa
ripoti za hivi karibuni zimebainisha kuwa dunia nzima inapoteza jumla ya
dola bilioni 400 kwa mwaka kwa njia ya wizi wa mitandaoni hivyo
kushindwa kulinda mitandao ya mawasiliano kunapelekea hasara kubwa kwa
Taifa na Dunia kwa ujumla.
Naye Afisa Mwandamizi wa ufundi na
ushauri wa Shirika la Mawasiliano la Jumuiya ya madola , Fargani
Tambeayuk amesema kuwa Jumuiya hiyo inawasaidia nchi wanachama katika
kudhibiti usalama wa mitandao ili kusaidia nchi hizo kupata maendeleo
kwa kutumia mitandao pamoja ma kuepukana na uhalifu.
Kwa upande wake Mratibu Mwandamizi
wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Makosa ya mitandao, Joshua Mwangasa
amesisitiza suala la kutolewa kwa elimu ya usalama wa mitandao liwe
endelevu akiamini kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuepuka kutumia
vibaya mitandao ya mawasiliano.
Aidha, ameusifia mpango huo kwani
utawasaidia Jeshi la Polisi kuweza kukabiliana kirahisi na wananchi
wanaofanya makosa kwenye mitandao pia amesisitiza kuwa makosa ya
kimtandao ni kama makosa mengine hivyo taratibu za kuripoti makosa hayo
ni zile zile za kawaida.
Tags
HABARI KITAIFA