Na Georgina Misama-MAELEZO
Mpaka kufikia 2021 serikali
imeahidi kusambaza umeme wa kutosha na wa uhakika katika vijiji vyote
nchini ili kuendana na dhamira ya kuelekea katika uchumi wa kati kupitia
viwanda.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo wakati wa kipindi cha
TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa ya TBC1 kwa
ushirikiano na Idara ya Habari-MAELEZO.
Prof. Muhongo alisema kuwa
kukamilika kwa miradi ya kuzalisha nishati ya umeme ikiwemo Mradi wa
Kinyerezi 1 unaozalisha megawati 150 kwa siku umesaidia kuongeza
upatikanaji wa huduma ya umeme wa kutosha mijini na baadhi ya vijiji.
“serikali sasa ipo katika
kutekeleza miradi mikubwa ya nishati za umeme na gesi ikiwa ni jitihada
za kuhakikisha mpaka kufikia 2021 vijiji vyote nchini viwe vimepata
huduma ya nishati ya umeme”. Alisema Prof. Muhongo
Aidha, Prof. Muhongo alisema kuwa
utekelezaji wa Miradi hiyo unaenda sambamba na lengo la Serikali ya
awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya
kuthibiti utoroshaji wa madini nchini Prof. Muhongo alisema kuwa
serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwakamata watoroshaji wa madini
hasa katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege.
Prof. Muhungo alisema kuwa kuanzia
mwaka 2012 wamekamata madini ya aina mbalimbali zaidi ya Tani 10
yaliyokuwa yanatoroshwa kutoka nchini kwenda nchi mbalimbali.
Prof. Muhongo amewataka watanzania
kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na utekelezaji wa miradi katika
sekta ya gesi na mafuta ili kujiongezea kipato na kuiwezesha nchi
kutimiza malengo yake kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Tags
HABARI KITAIFA