BANDA MEDIA BLOG

Martin Saanya ni chaguo sahihi Yanga v Simba?

martin-saanya
Na Baraka Mbolembole
Pambano la mahasimu wa soka nchini Yanga SC na Simba SC litapigwa siku ya Jumamosi hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo kongwe na kubwa zaidi Tanzania zitavaana katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu Tanzania Bara msimu.

Simba haijapoteza mchezo wowote hadi sasa kufikia raundi ya 6, wakati mabingwa mara mbili mfululizo na watetezi wa taji hilo, Yanga ilikubali kuangusha pointi 3 za kwanza msimu huu walipochapwa 1-0 na Stand United ya Shinyanga siku ya Jumapili iliyopita.
Simba wana alama 16 baada ya kucheza game sita na Yanga wana pointi 10 baada ya kucheza game tano.
Mwamuzi Martin Saanya kutoka Mkoani Morogoro atachezesha pambano lake la tatu la mahasimu hao wa Dar es Salaam huku likitaraji kuwa pambano lake la Tano linalowakutanisha timu za mji mmoja ‘Pacha.’
Saanya ni chaguo sahihi na bora katika game ya Jumamosi hii. Ni mwamuzi mwenye uwezo wa kutoa maamuzi na kuyasimamia bila uoga jambo ambalo wakati mwingine huwashinda waamuzi wengi. Saanya aliwahi kufungiwa kuchezesha soka kwa muda wa mwaka mmoja mwaka 2012.
Nakumbuka adhabu yake niliipinga kwa maana alifungiwa kwa sababu tu alikubali mkwaju halali wa penati ambao Coastal Union waliupata dakika ya 89′ na kusawazisha katika pambano la sare ya kufungana 1-1 vs Yanga katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Saanya alitoa mkwaju wa penati kwa Coastal kufuatia mlinzi wa Yanga kuunawa mpira uliokuwa umepigwa kuelekea golini mwao. Wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo walikasirishwa na uamuzi wa refa huyo lakini bado alisimamia uamuzi wake na Jery Santo akafunga.
Saanya ana uwezo mzuri wa kuusoma mchezo na kuwatambua wachezaji vile wanavyocheza, ana kasi ambayo mara nyingi humsaidia kuwa karibu na mpira hivyo huweza kuyaona matukio mengi, anapendelea kutoa kadi ikiwa ataona mchezaji husika anataka kuharibu mechi.
Pambano lake la kwanza la ‘Dar es Salaam Pacha’ lilimalizika kwa Yanga kuifunga Simba 2-0 siku ya mwisho ya msimu wa 2013/14.
Nakumbuka katika mchezo ambao Simba iliwatumia kundi kubwa la vijana waliokuwa wamepandishwa timu ya kwanza na kocha, Mfaransa, Patrick Liewig mwamuzi huyo aliumia na kulazimika kutibiwa kwa dakika kadhaa kufuatia kugongwa maeneo ya puani wakati akiamulia ugomvi wa wachezaji, Nassoro Chollo na Didier Kavumbagu.
Ukiachana na tukio hilo, Saanya alikuwa katika kiwango bora kiuchezeshaji.  Akachezesha pambaoo la Ngao ya Jamii baina ya Yanga vs Azam FC miezi michache baadae na akalimudu pambano hilo lingine kubwa katika soka la Tanzania.
Machi, 2015, Saanya akaonyesha ubora wake kiuchezeshaji wakati alipochezesha game yake ya pili ya ‘Watani  hao wa Jadi.’ Simba ilishinda 1-0 katika mchezo huo kwa goli la mkwaju wa mbali la mganda, Emmanuel Okwi.
Saanya anapenda wachezaji wanaocheza mchezo wa kiungwana kwa wenzao na mwepesi wa kutoa kadi za manjano ikiwa wachezaji watacheza kwa lengo la kuharibu mchezo.
Mwamuzi ni mtu muhimu kuliko wote ndani ya dakika 90′ za mchezo wa kandanda na Saanya hayuko tayari kushindwa na baadhi ya wachezaji wasio waungwana ili kuifanya mechi iwe salama na wapenzi wafurahie mpira.
Saanya ni chaguo zuri la mwamuzi ambalo Bodi ya ligi imelifanya. Kwa wachezaji wanapaswa kutambua kwamba wanakwenda kusimamiwa na mtu mwenye kujiamini, mwenye kusimamia maamuzi yake na anayependelea soka la kiungwana.
Mwamuzi huyu anapenda sana kutumia kadi kama njia ya kulinda ubora wake na ubora wa mchezo husika.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG