Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Magufuli amesema kuwa huu ni wakati
mwafaka kwa muswada wa sheria ya huduma za vyombo vya habari
kukubaliwa na kuwa sheria kwa vile tasnia ya habari inakumbwa na
changamoto nyingi zitakazotatuliwa na sheria hiyo.
Akizungumza na wahariri pamoja na
waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari leo, Ikulu jijini Dar es
Salaam Rais Magufuli alisema kuwa muswada huo ni wa muda mrefu na sasa
ni wakati mwafaka kwa vile tansia ya habari inakumbwa na changamoto
nyingi zinazoweza kutatuliwa na muswada huo.
“Hii sheria ya huduma za vyombo
vya habari imechelewa kwa vile mchakato wake ulianza tangu mwaka 2011
hadi sasa mwaka 2016 wadau walikuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa na
kutoa maoni yao ambayo yangeweza kuboresha muswada huo” alisema Rais
Magufuli
Ameongeza kuwa, Sheria hii
italeta mabadiliko katika tasnia ya habari kwa vile kutakuwepo na Bodi
ambayo itashughulikia masuala ya taaluma ya habari, pamoja na mambo
mengine yaliyoanishwa katika muswada huo ambayo ni maslahi ya waandishi
wa habari nchini.
Muswada huu unatazamiwa
kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kufanyakazi kitaalamu
kwa kuandika na kutangaza habari zenye ukweli zitakazochangia katika
harakati za kuleta maendeleo kwa nia ya kuwasaidia watanzania na
serikali kwa ujumla katika kufikia malengo yake.
Muswada wa Sheria ya huduma za
habari umesomwa leo Novemba 4, 2016 katika kikao cha tano cha Bunge
na mkutano wa 11, ambapo utajadiliwa na kufuata taratibu zingine kabla
ya kuwa sheria.
Tags
HARUSI & SHEREHE