BANDA MEDIA BLOG

WALIOFAULU NI LAZIMA WAENDE SEKONDARI – MAJALIWA


*Asema atafuatilia ajue kwa nini kuna tozo kwenye maghala ya Serikali

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.

“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema ni wanafunzi wanaenda shule za msingi kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto sasa iweje watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari. “Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” amesema.

Amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa wamechelewa.

“Kama tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri kuwa ,tutapata Vijana wengi watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.”

“Tafuteni moja kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG