Mh mkuu wa mkoa wa Arusha
Mrisho Mashaka Gambo amefanya ziara katika chuo kikuu cha Arusha. Katika
ziara hiyo Mkuu wa mkoa amezungumza na uongozi wa chuo,watumishi pamoja
na wanafunzi.
Pia alipata fursa ya kutembelea miundo mbinu mbali mbali ya chuo hicho ambacho kinamilikiwa na kanisa la Waadventista Wasabato.
Alipata muda wa kuzungumza na
wanafunzi na kusikiliza kero zao na changamoto zinazowakabili ikiwemo
kutokuridhishwa na huduma zinazotolewa na mfuko wa Bima ya Afya katika
utoaji wa kadi za Bima ya Afya hivyo kusababisha usumbufu mkubwa wakati
wa utoaji wa huduma hiyo chuoni hapo.
Masuala mengine ni kama tatizo
la kukatika umeme mara kwa mara, tatizo la maji, ulinzi na usalama
chuoni hapo, sehemu kubwa ya wenye sifa ya kukopeshwa na bodi ya mikopo
kutokuipata mikopo hiyo, pia wamemweleza hofu yao ya kumaliza masomo na
kukosa ajira.
Katika kujibu changamoto hizo
mkuu wa mkoa ameuagiza uongozi wa NHIF (bima ya Afya) mkoa wa Arusha
kufika chuoni hapo mara moja ili kuweza kulitatua tatizo hilo ndani ya
wiki moja toka leo.
Mkuu wa mkoa ametoa maagizo kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, mkuu wa wilaya ya Arumeru Ndg.
Alexander Mnyeti na Mhandisi wa maji wilaya ya Arumeru kufika chuoni
hapo siku ya Jumatano tarehe 01/02/2017 na kukaa na uongozi wa chuo
kuona namna wanaitatua kero hiyo ya maji ya muda mrefu.
Kuhusiana na suala la ulinzi
chuoni hapo na maeneo ya jirani Mh. Mkuu wa mkoa ameihamasisha jamii
nzima ya Arumeru bila kuwasahau wanachuo wenyewe kuona namna gani
wanaweza kujenga kituo cha polisi ili kuimarisha usalama chuoni hapo na
maeneo ya jirani, kwa kuanzia Mh. Gambo ametoa mabati 100 ili kuamsha
ari ya wananchi na jamii nzima ya Arusha University kuanza ujenzi huo
mara moja.
Mh. Gambo ameichukua hoja ya
wanafunzi walio na sifa za kukosa mkopo na kuagiza uongozi wa chuo kumpa
majina ya wanafunzi husika na ofisi yake kuyawasilisha bodi ya mikopo
ili yashughulikiwe, pia ametoa changamoto kwa vyuo kutoa kozi kulingana
na mahitaji ya serikali kwa wakati husika ili kuepusha mgogoro wa kuwa
na wahitimu wengi wasio na ajira.
Vile vile katika kujibu baadhi
ya changamoto Mh Gambo aliwapongeza wanafunzi kwa ujasiri wa kutoa kero
zao bila woga na ameahidi ataweka utaratibu wa kutembelea vyuo vikuu
vilivyopo mkoani Arusha ili kujua mazingira halisi na matatizo
yanayokabili vyuo husika.
Tags
ELIMU