Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna
Mstaafu Zelote Stephen amesema kuwa Mkoa hauna njaa baada ya kufanya
ziara katika maghala mbalimbali ya wajasiriamali pamoja na kiwanda cha
Unga cha Energy Mills vyote vilivyopo katika mji wa Sumbawanga.
“Mmejionea wenyewe, Katika
Manispaa ya Sumbawanga suala la kwamba hakuna chakula ama kuna njaa ni
maneno hewa, hakuna kitu kama hicho, Chakula kipo cha kutosha nafaka
karibu zote zipo,” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.
Ameongeza kuwa wakulima wengi
wameonekana kuuza mazo yao kwa wachuuzi na kusababisha wafanyabiashara
wa masokoni kwenda kununua mazao hayo kwa bei na matokeo yake naoi li
wapate faida nao wanaongeza bei jambo linalosababisha wananchi kushindwa
kununua na wao kulalamika kuwa hakuna wateja.
Katika suala la malalamiko ya
wananchi kuosa pesa Zelote Stephen alifafanua “malalamiko yaliyokuwepo
kuwa pesa hakuna, nami nakubali, kipindi hiki tulichopo ni wakati wa
kilimo na wakati wa kilimo maana yake kila mtu yupo shambani, na mwezi
ujao (Februari) kuanzia tarehe 20, kuna taarifa kwamba watu wataanza
kuvuna maharage, kwahiyo ni dhahiri kwamba suala la njaa na bei hakuna
mtu ambae atalizungumzia.”
Katika kulishuhudia hilo mmiliki
wa kiwanda cha Energy Mills, Aziz Tawakali alisema kuwa mpaka sasa
katika ghala lake ana tani 30 na mifuko 3400 ya unga wa sembe wenye kilo
50 kwa kila mfuko, na kuongeza kuwa kwa idadi hiyo kiwanda chake
kinaweza kufanya biashara hadi mwezi wa tatu mwaka huu.
“Sio kwamba kuna njaa, na katika
mwaka mzima hatujawahi kukosa stock ya chakula, na wa stock hii
niliyonayo nina uwezo wa kuuza mpaka mwezi wa tatu” Azizi alithibitisha.
Nae mmoja wa wamiliki wa mashine
za mpunga Mathias James amethibitisha kuwa katika Mkoa wa Rukwa hakuna
shida ya chakula bali shida iliyopo ni ya wateja wa kununua chakula
hicho, hivyo aliwaasa wale wote wanaosema kuwa hawana chakula cha
kununua wafike katika ofisi yake.
“Kusema kuwa kuna njaa, hiyo si
kweli, maana sisi tunahangaika kutafuta wateja, na wateja tunaowategemea
ni kutoka Mbeya na Tunduma na wengine kutoka nchi za jirani kama Zambia
na Kongo, hivyo tunawaasa wale wanaotafuta mchele, kwetu upo, tuna
magunia ya mpungaya kilo 90 zaidi ya 18,000 hayana wateja, mpunga upo,
mahindi yapo, waohitaji watuone,” Mathias alisisitiza.
Nao baadhi ya wajasiriamali wadogo
wadogo wanouza kwa visado nao pia waliendelea kulalamikia upungufu wa
fedha katika mifuko yao na kuongeza kuwa shida za wananchi si chakula
kwa sasa bali pesa ndio ngumu na ndio inayotusababishia njaa.
“Njaa yetu pesa hakuna chakula
kipo ila hela ya kununulia hayo mahindi ndio hakuna, kutokana na
mzunguko wa biashara hela hakuna ila chakula kipo,” Deus Malonga
alisema.
Nae Agness Palakata alisema “Tokea
asubuhi tunauza hilo gunia halijaisha, sasa namna hii hatuwezi kurudi
nyumbani uawalisha watoto, pesa hakuna, chakula kipo ila pesa ndio
tatizo, shida yetu na njaa yetu ni pesa.”
Kwa kuthibitisha kutokuwepo kwa
njaa Zelote Stephen aliongeza kuwa wakala wa taifa wa hifadhi ya
chakula (NFRA) wana jumla ya tani 15,500 ambazo zipo kwenye magala yao.
Kaimu Afisa Habari Mkoa wa Rukwa
Abdulrahman Salim.
17/01/2017.
Tags
HABARI KITAIFA