Jitihada za uokoaji zikiendelea Baadhi ya wafanyakazi wa Mgodi wa RZ wakishiriki kutoa vyuma kwenye eneo lililofukiwa
Mashine ya kutolea udongo uliojifukia ikiendelea na juhudi za kufukua ili kupata sehemu ya mlango wa kutokea.
Bomba za kupitisha Hewa ya OXJEN ikiwa imepitishwa chini kwa chini.
Mtambo unaopeleka hewa ukiangaliwa kwa makini.
…………
IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE
NI SIKU ya pili sasa tangu
wachimbaji kumi na nne (14) ambapo simanzi, masikitiko yameendelea
kutanda baina ya jamii na ndugu wa wachimbaji ambao wamefukiwa na udogo
kwenye Mgodi wa RZ uliopo Kijiji cha Nyarugusu Wilaya ya Geita hata
hivyo jitihada na zoezi la kuwaokoa bado linaendelea .
Zoezi la uokoaji linalosimamiwa na
kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, Ofisi ya Madini Kanda ya ziwa
magharibi ikiyashirikisha makampuni ya Migodi ikiwemo GGM na Busolwa
mine, imeelezwa hatua iliyofikiwa hadi leo saa 1:30 asubuhi walikuwa
wamechimba takribani mita 20 kati ya 30 ili kuwafikia wachimbaji hao.
Kufuatia hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga aliwataka ndugu na
jamaa wa watu 14 waliofukiwa na kifusi ndani ya Mgodi wa RZ kuwa na
subira wakati waokoaji wakiendelea na Zoezi hilo.
“Mimi niwatake ndugu na jamaa
kuendelea kuvuta subira wakati waokoaji wakiendelea na kutumia mashine
kwa ajili ya kuwaokoa watu waliozama chini ya Mgodi huo jambo ambalo
hata Mkoa wa Geita umelipokea kwa masikitiko makubwa sana,’’alisema
Kyunga.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ametoa
kalipio kali kwa wawekezaji ambao hawajali ustawi wa wafanyakazi wake
kwa uzembe ambao unaweza kuepukika na kwamba alisikitishwa sana namna
mgodi wa RZ ambavyo ulikuwa haujali masuala ya miundombinu yake.
ZOEZI la uokoaji limeendelea huku
matumaini ya wengi yakizidi kupotea kutokana na ugumu wa kazi dalili
hata kidogo hazionekani lakini kamishina wa madini kanda ya ziwa
magharibi Bw. Yahaya Samamba amesema zoezi hilo litakamilika na watu
watakuwa salama kutokana na hewa wanayoipata kupitia mpira unaoingiza
kwa kutumia mashine.
Maduka online usiku kucha
imeshuhudia hatua kwa hatua zoezi hilo, licha ya baadhi ya maafisa wa
serikali wakishindwa kuvumilia kukesha kwenye zoezi hilo.
Kamishina msaidizi wa madini
kanda ya Ziwa Yahaya Samamba ameendelea kuelezea kuwa pamoja na kuunda
kamati ya uokoji wamekutana na changamoto kubwa kwa sababu ya duara
walikozama watu hao kuwa chini ya kilomita 35.huku akisema wanaendelea
kuomba mashine nyingine kutoka kwa makampuni mengine kama zoezi
litaonekana kuwa na ugumu.
“Tumeunda kamati ya uokoji na
kamati yetu imehusisha makampuni yote yalioleta mashine zao kwa ajili ya
uokoaji huo huku naye akiwataka wananchi kutoanza kutoa lawama kwa
baadhi ya vyombo vya Serikali na ngazi nyingine kwenye wizara ya
madini,, alisema Samamba.
Maduka online ilibahatika
kukutana uso kwa uso na diwani wa kata ya Nyarugusu yalipo maafa hayo,
Swalehe Juma alisema janga hilo limemnyima usingizi na kwamba siku ya
jana alilazimika kukesha na waokoaji.
“Mwandishi nakushukuru kwa kuwa
nasi kwenye zoezi hili ni kweli mimi nyumbani ni karibu hata kwa miguu
naweza kutembea nikafika lakini siwezi kwenda jambo hili limeninyima
raha nitawezaje kwenda kwangu wananchi wangu wako ndani ya
shimo,’’alisema Juma.
Hata hivyo baadhi ya wananchi
waliohudhuria kushuhudia tukio hili la aina yake katika wilaya ya Geita
ikiwa ni mwanzoni mwa mwaka wa 2017, walisema lawama kubwa wanazielekeza
kwa mamlaka za madini kwa kushindwa kujisimamia katika kuhakikisha
uchimbaji ulio imara kwenye migodi unaboreshwa.
“kaka hili jambo linasikitisha
sana hebu fikiria tangu usiku wa tarehe 26 saa saba usiku mpaka leo siku
nyingine ya tarehe 27 tumekutana tena watu wako ndani ya kifusi je
watapona licha ya matumaini tunayopewa…Mimi hapa naelekeza lawama kwa
ofisi ya Madini Mkoa wa Geita hawakagui migodi ipasavyo,’’alisema Mkazi
wa Nyarugusu Saidi Mrisho.
“Kwanza nashangaa nilimsikia jana
kamishina wa madini kanda ya ziwa akisema chanzo ni kutokana na miti
iliyokuwa imeshikilia ukuta kuwa imeoza sasa hapa najiuliza je, kazi ya
ofisi ya madini nini wanakagua nini na je waliwahi kuwaambia kuwa miti
hii haifai katika ukaguzi wao inapaswa serikali nayo iwachukulie hatua
kubwa kwa uzembe huu haiwezekani,’’alisisitiza.
Katika shughuli za uokoaji
wananchi hawakuacha kuipongeza kampuni ya uchimbaji wa madini ya Busolwa
Mine inayomilikiwa na mwekezaji mzawa Baraka kwa kujitolea mashine zake
za greda kuhakikisha wanafanikisha adhima ya kuwaokoa watanzania 13
pamoja na raia wa china Bw. Meng Juping, ambaye anadaiwa hakuwa na redio
koll kama ilivyokuwa kawaida yake wakati anakwenda kutekeleza majukumu
yake ya uzalishaji wa madini ya dhahabu.
Hata hivyo Madukaonline
ilishuhudia kikosi cha zima moto na uokoaji Mkoa wa Geita pamoja na
jeshi la polisi wakiendelea na majukumu yao ya kuhakikisha eneo hilo
liko salama.
Tags
HABARI KITAIFA