MWANAFUNZI
wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Milundikwa iliyoko
katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa mwenye umri wa miaka 15 (jina
limehifadhiwa), mkazi wa Kijiji cha Katani, amenusurika kufa baada ya
kunywa aina saba za dawa kwa lengo la kujiua akidaiwa hataki shule.
Akizungumza
jana eneo la tukio, mama mzazi wa mtoto huyo, Stella Hamis alisema juzi
saa 2:00 asubuhi, alimfokea mtoto wake huyo baada ya kumuona nyumbani
badala ya kwenda shule.
Stella alisema alimtaka mwanawe aende shule mara moja naye akaelekea shambani.
Hata
hivyo, alisema baada ya muda mfupi, mtoto wake huyo alijifungia ndani
na kunywa dawa za hospitalini aina saba tofauti zilizokuwapo na kuandaa
kamba kwa ajili ya kujinyonga.
"Lakini
kwa bahati mmoja wa wana familia, aliingia ndani ya nyumba hiyo na
kumkuta mtoto huyo akiwa hajiwezi kutokana na dawa alizokunywa,"
alisema.
Stella
alisema taarifa zilisambaa kwa jirani ambao walifika eneo la tukio la
kumchukua mtoto huyo na kumpeleka zahanati ya kijiji kwa matibabu.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Solana Kazikodi, alithitibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kazidosi
alisema ofisi yake ilipata taarifa mapema juu ya tukio hilo na ndiyo
waliofanya kazi ya ziada kuhakikisha mtoto huyo anakimbizwa haraka
katika zahanati yao ya kijiji.
Alisema
mtoto huyo alifaulu kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kufanya
vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Katani.
Hata hivyo, alisema tangu aripoti katika shule hiyo, mahudhurio yake yamekuwa ni hafifu kutokana na kutopenda kusoma.
Mganga
wa zahanati hiyo, Godfrey Manga, alithibitisha kumpokea mwanafunzi huyo
na kwamba alipatiwa matibabu na hakuathiriwa kwa kiwango kikubwa na
dawa hizo kwa kuwa walimuwahisha zahanati kupata huduma.
Tags
UKATILI
