KUNA baadhi ya mambo ambayo mara nyingi ukiyafanya huwa ni lazima
ufupishe maisha yako kwa namna moja au nyingine. Hii yote huwa inatokana
na aina ya maisha uliyoyachagua, ambayo huwa ni hatari kwa afya na
maisha kwa ujumla. Watu wengi wana tatizo la kuishi maisha ya kujisahau
na kufanya vitu ambavyo ni hatari. Haya ni baadhi ya mambo ambayo
ukipendelea kuyafanya basi maisha yako yanakuwa hatarini.
Kula bila mpangilio
Watu wengi huwa wanaishi maisha ya kutojali afya zao. Yapo mambo ambayo
ukiyafanya afya yako inakuwa hatarini moja kwa moja hata kama hujasomea
udaktari ni rahisi kwako kuyafahamu.
Mfano kama unapenda kula vyakula bila mpangilio na vibovu ambavyo
havifai, ni lazima afya yako itakuwa hatarini. Lakini si hivyo tu, kama
wewe ni mvutaji mzuri wa sigara au unakunywa pombe kupita kiasi bila
utaratibu, ni rahisi mno kwako kuweza kuharibia afya yako na hivyo
kuyafanya maisha yako kuwa hatarini.
Maisha ya upweke
Hakuna kitu hatari katika maisha yako kama kuamua kuishi wewe kama wewe.
Hili ni jambo la hatari mno kwako na kwa namna yoyote ile linaweza
kuhatarisha afya yako. Kwa kawaida binadamu ameumbwa ili kuweza kuwa na
uhusiano na wengine. Sasa wapo watu ambao hawana uhusiano mzuri na
wengine kwa sehemu kubwa.
Watu hawa kutokana na kutokujihusisha kwao na watu wengine hujikuta
wakiwa na maisha magumu. Muda mwingi mawazo yao huwa ni hasi kutokana
na kujitenga na hivyo hujikuta ni watu wa kuwa na msongo wa mawazo,
hivyo huwa ni rahisi kwao kupoteza maisha.
Kukaa chini muda mrefu
Hili ni jambo dogo tu, na unaweza ukalichukulia kwa urahisi, lakini
wataalamu wa afya wanaonya jambo hili kwa kuwa linaweza kuathiri afya.
Inashauriwa kuwa si vizuri kukaa chini kwa muda mrefu bila ya kusimama.
Hiyo inaweza kukusababishia magonjwa kadhaa ikiwamo uti wa mgongo.
Ili kuweza kulinda afya yako na kuwa bora zaidi unapaswa kuepuka kukaa
chini kwa muda mrefu. Kama una kazi ambayo inakulazimu ukae chini muda
mrefu basi jitahidini angalau uwe unasimama kila baada ya dakika 45 ili
kufanya mzunguko wa damu uendelee vizuri.
Kuangalia runinga kwa muda mrefu
Wataalamu wa afya wanabainisha kuwa kuangalia TV kwa muda mrefu tena
ukiwa karibu nayo unaweza kuua baadhi ya seli ndani ya mwili. Kwa upande
wa wanaume tafiti zinaonyesha kuwa kuangalia TV kwa muda mrefu
hupunguza uwezekano wa kuzalisha mbegu za kiume kwa asilimia kubwa.
Kikubwa cha kuzingatia hapa ni kutambua kuwa kuangalia runinga kwa muda
mrefu kwa namna moja au nyingine kuna madhara ambayo unaweza usiyaone
kwa urahisi.
Kutopata usingizi wa kutosha
Kukosa usingizi ni tatizo ambalo linaiweka afya yako hatarini moja kwa
moja. Kwa kawaida binadamu anatakiwa alale saa 8 kwa siku. Unapokosa
kulala saa hizo unaweza kupoteza kumbukumbu taratibu.
Lakini si hivyo tu, pia hukusababishia kupata tatizo la akili. Kwa hiyo, usingizi ni jambo muhimu mno kwa afya yako.
Tags
AFYA
