WAKATI
jiji la Dar es Salaam likiwa katika mapambano ya kukabiliwa na dawa za
kulevya jiji hilo limekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu ambapo mtu
mmoja aliyetajwa kwa jina la Ramadhan Kiumbo (maarufu kwa jina la Popo)
mkazi wa Kibada Kigamboni amefariki kutokana na ugonjwa huo.
Akizungumza
Dar es Salaam leo ndugu yake na marehemu huyo aliyejitambulisha kwa
jina moja la Issa alisema ndugu yao huyo alifariki jana wakati akipatiwa
matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni ya Vijibweni.
“Ndugu
yetu amefariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na amezikwa leo
‘jana’ na Halmshauri ya Wilaya ya Kigamboni katika makaburi ya Serikali
ya Kisiwani na kuhudhuriwa na ndugu wachache” alisema Issa.
Issa
aliongeza kuwa katika Hospitali hiyo kuna wagonjwa 12 wanaotibiwa
ugonjwa huo na tayari imeanzishwa kambi maalumu ya wagonjwa hao katika
hospitali hiyo ya Vijibweni.
Alisema
kutokana na kuibuka kwa ugonjwa huo shule zote za Halmashauri ya
Kigamboni zilifungwa siku ya Ijumaa kwa hofu ya wanafunzi kupata
maambukizi.
“Siku
ya Ijumaa wanafunzi walirudishwa nyumbani na tulipowauliza walisema
shule zimefungwa kutokana na ugonjwa wa kipindupindu” alisema Issa.
Baadhi ya maeneo ambayo yametajwa kuwa na ugonjwa huo ni pamoja na Vingunguti na Temeke.
Mkuu
wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa alithibitisha kuwepo kwa
ugonjwa huo ndani ya manispaa yake ambapo mtu mmoja ameshafariki huku
wengine wakiwa Hospitalini wakipatiwa matibabu.
”
Ni kweli ugonjwa huu umeingia lakini tumefanya uchunguzi na kugundua
umeanzia sehemu moja inaitwa Kichangani ambapo watu wote ambao wameletwa
Hospitali waliupatia eneo hilo walipoenda kwenye msiba.
”
Lakini tayari maofisa wetu wa afya wameshachukua hatua za awali za
kukabiliana na ugonjwa huu kwa kutembelea nyumba za wagonjwa hao na
kupulizia dawa ili kuweza kuzuia maambukizi kwa watu wengine,” alisema
Mgandilwa.
Tags
AFYA