Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing amesema tofauti kati ya Serikali
ya Tanzania na ubalozi wa China umesababisha kukwama kwa ujenzi wa
Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Mchakato wa ujenzi wa bandari hiyo ulianza kipindi cha Awamu ya Nne ya
uongozi wa Rais Jakaya Kikwete na ulitarajiwa kuhusisha Serikali za
Tanzania, China na Oman.
Akizungumza katika mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari juzi
jijini Dar es Salaam, Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema,
“Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na ukanda wa viwanda wilayani humo ni
uwekezaji mkubwa kati ya China na Tanzania katika miaka ya karibuni na
umeorodheshwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2016/17-2020/21).
“Kutokana na umuhimu wake unaohusisha Serikali za Tanzania, China na
Oman, ushirikiano kati ya maofisa kutoka idara za Serikali ya Tanzania
na ubalozi wa China wanazishauri pande zinazohusika kukunjua moyo na
kumaliza tofauti ili uweze kuendelea kukiwa na makubaliano kwenye mambo
ya msingi,” alisema Lu.
Hata hivyo, kwa sasa jitihada zinafanywa ili ikiwezekana makubaliano
hayo katika nusu ya mwaka huu na ujenzi uanze ndani ya mwaka huu.
Akizungumzia hilo kwa njia ya simu jana, Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alikiri kutofatiana na Wachina
katika ujenzi huo.
“Unajua vitu vingine mnapenda kuvikuza bila sababu. Sisi tuliiruhusu
Serikali ya China kujenga Bandari ya Bagamoyo kwa kitu kinachoitwa PPP
na ule ujenzi ulikuwa na mambo mengi kama maeneo ya viwanda ili kupata
uhakika wa mizigo. Wachina wakatuletea kampuni kwamba sasa ongeeni na
kampuni hii, tukawa tunaongea tunaangalia terms au unataka tuwape hivi
hivi? Alihoji.
Waziri Ngonyani alisema baadaye Wachina walileta Serikali ya Oman kwenye mradi huo.
“Hivyo vingine vyote wanatafuta tu sababu ya kutuchelewesha. Mara ya
mwisho tumewaambia lazima yale maeneo tuliyobishania tukubaliane ifikapo
Februari 28. Kwa hiyo tunatarajia kupata taarifa ya mwisho ya ujenzi wa
bandari hiyo kutoka kwa contractors wa China na Oman,” alisema.
Tags
MIUNDOMBINU
