MBUNGE wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) amepongeza viongozi wa Serikali kwa jinsi wanavyojali na kuhudumia wananchi.
Alitoa pongezi hizo juzi kwenye mikutano miwili ya hadhara Orkesumet na
Mirerani wilayani hapa, baada ya kupewa nafasi kusalimia wananchi kabla
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajazungumza nao.
“Serikali hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri Mkuu. Kwa mara ya
kwanza katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia mradi wa
maji kutoka Mto Ruvu unaoendelea kujengwa sasa,” alisema akiwa
Orkesumet.
Alitumia fursa hiyo kumwomba Waziri Mkuu afuatilie ujenzi wa hospitali
ya wilaya, kwani sasa wanategemea kituo cha afya na hali ikibadilika
inabidi mgonjwa apelekwe Arusha Mjini umbali wa kilometa 150 kutoka
hapo yalipo makao makuu ya wilaya.
Pia aliomba ijengwe barabara ya lami kuunganisha wilaya hiyo wilaya za Hai na Kiteto.
Akiwa Mererani, Ole Millya aliipongeza Serikali kwa kujenga barabara ya
lami kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mererani. Hata
hivyo, aliiomba Serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze kufika
Mirerani na Orkesumet.
Akijibu maombi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza Mbunge huyo kwa
uungwana wake wa kutambua juhudi za Serikali kwa wananchi wa jimbo lake.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani
Manyara, aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya nao
kazi bila kubagua kwa itikadi za kisiasa.
Tags
SIASA
